Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatua zachukuliwa kuokoa hifadhi ya Makere kwa kupanda miti

7120d9a403bbffa546e5b2516cdaf8be Hatua zachukuliwa kuokoa hifadhi ya Makere kwa kupanda miti

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFUKO wa Misitu Tanzania (TaFF) kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamejiwekea lengo la kupanda miti katika hekta 30,000 za msitu wa hifadhi Makere kusini uliopo wilaya ya Kasulu, Kigoma.

Katibu Tawala wa mfuko huo, Dk Tuli Msuya alisema upandaji wa miti ni sehemu ya ubadilishaji wa mfumo uliokuwepo wa msitu wa asili kuwa msitu wa serikali ili kupunguza uharibifu kwenye misitu ya asili na utegemezi wa miti ya asili.

Naye Kamishna Mkuu wa Uhifadhi (TFS), Profesa Dos Santos Silayo alisema upandaji huo wa miti utaokoa hifadhi hiyo yenye ukubwa wa hekta 64,000, lakini nusu yake ikiwa imeharibiwa kwa miaka mingi kwa shughuli za kilimo pamoja na makazi ya wakimbizi.

Wilaya ya Kasulu ni makazi ya wakimbizi walioingia nchini kuanzia miaka 1964, 1974 na miaka ya karibuni wanaofikia 130,000. Wakimbizi hao pamoja na wananchi wamekuwa wakifanya shughuli za kilimo katika msitu huo.

Profesa Silayo alisema Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) umeamua kutafuta suluhu katika changamoto ya uhifadhi wa mazingira katika msitu wa Makere kwa sababu ni chanzo cha maji cha mto Malagalasi unaoingia Ziwa Tanganyika.

Profesa Silayo alisema: “Tumeona tuokoe mazingira ya msitu huu kwa kupanda miti ya aina mbalimbali na tuwezeshe kilimo biashara katika eneo hili. Kilimo hiki kitasaidia katika upatikanaji na kuni na malighafi nyingine.”

Mhifadhi Misitu, Dorisia Kashura alisema watahakikisha upandaji miti huo unamalizika kwa kwa wakati.

Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kasulu, Shadrack Msilu alisema wamepanda asilimia 30 ya miti inayotakiwa kwa wakati huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz