Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hatari! Mimba za watoto zageuzwa mtaji wa wazazi

B0d76cef74722d92444b3330fcf2ac38 Hatari! Mimba za watoto zageuzwa mtaji wa wazazi

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“SUALA la mimba, sheria ni kali. Kesi za mimba zinakuwa za mazoea na kesi nyingi hazi? ki mwisho, wengi hawako tayari kusimama mahakamani kutoa ushahidi hivyo wamaamua kumalizana kifamilia.” Maneno hayo yanasemwa na Ofisa Elimu Taaluma Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Msingwa Ibrahim wakati wa kikao cha kupanga mikakati wa kutekeleza mradi wa kudhibiti mimba, ndoa za utotoni na kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Mradi huo unatekelezwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Woman Wake Up (WOWAP) kwa ufadhili wa taasisi ya The Foundation for Civil Society. Ibrahim anasema kumekuwa na matukio mengi ya wanafunzi kupata mimba lakini ushirikiano unakuwa mdogo hali inayosababisha haki isitendeke na hivyo kuchangia mabinti wengi kukatisha masomo na kushindwa kutumiza ndoto zao.

Anasema licha ya sheria kuwa kali, kesi za mimba zimekuwa kama suala la mazoea katika jamii, kwani wanafunzi wanaopata mimba hawatoi ushirikiano ili wahusika wachukuliwe hatua.

Anabainisha kuwa kwa mwaka katika wilaya hiyo kesi za mimba huwa kati ya 60 na 70 lakini hakuna anayehukumiwa. Katika muktadha huo anasema kinachotakiwa ni kesi hizo kusimamiwa vizuri na wahusika kutoa ushirikiano.

“Utakuta mwanafunzi kapata ujauzito lakini anataja watu tofauti tofauti. Wakati mwingine mimba za wanafunzi kama mtaji wa wazazi, yaani mtoto ap ate mimba mzazi apate pesa,” anasema

Anasema kuna wanafunzi mara ya kwanza wanapopimwa wanakutwa na ujauzito, wakirudia kupimwa ujauzito hakuna kumbe wameshatoa na hivyo kukosa ushahidi.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Chamwino, Robert Kaombwe anasema kesi zikiwa mahakamani huwa hazifiki mwisho kutokana na kukosekana kwa ushirikiano, mashahidi hawafiki mahakamani baada ya kuamua kumalizana kifamilia.

Mkuu wa dawati la Jinsia la Polisi wilaya ya Chamwino, Levina Duwe anasema mpaka sasa kuna jumla ya kesi za mimba 58 zilizoripotiwa mwaka huu ambapo 53 ni za wanafunzi wa shule za sekondari na watano ni wa shule za msingi.

“Hii maana yake tumeshaongeza watoto wa mitaani. Mtoto ukikaa naye kirafiki anaonesha ana uchungu sana, turudi mashuleni, turudi kwa wazazi watoto hawana ndoto za mbele,” anasema

Anasema polisi inategemea ushirikiano wa mzazi vinginevyo inakuwa ngumu kumnasa mhalifu. “Mtoto kapewa ujauzito lakini anakuwa msiri kutaja mtuhumiwa anasema hamfahamu au katoroka, wanalipana wanaficha siri, wazazi wanakwamisha kesi, siwezi kupeleka jalada kwa mwanasheria wakati halina maelezo ya pande zote mbili,” anasema.

Mtendaji wa Kijiji cha Manchali, Mathew Sudi anasema kuna ulegelege mwingi unaosababisha kesi zisifike mwisho“Utakuwa mtuhumiwa anatoroka akirudi, anaishi pamoja na binti aliyepachikwa mimba,” anasema.

Anasema wakati mwingine taarifa inapofika kwa mtendaji, anapochukua hatua kwa mhusika jamii inaanza lawama na vitisho.

Anasema kuna uelewa mdogo wa wazazi na walezi juu ya haki za watoto wao na mustakabali wa Maisha yao ya baadaye.

Sudi anasema wakati mwingine matukio hayo huusishwa na imani za kishirikina na kwamba katika muktadha huo si kwa wanafunzi tu bali hata watu wazima hutendewa vitendo hivyo. “Manchali tuliwahi kupata kesi moja ya mama kufanya mapenzi na mtoto wake wa kumzaa kwa imani za kishirikina.

“Walipoanza mahusiano walikuwa wakitumia njia ya kawaida, lakini mtoto akaanza tabia ya kumlawiti mama yake, ndipo mama akapiga yowe watu wakajaa kijana alikamatwa, akafikishwa kituo cha polisi na akafunguliwa kesi mahakamani, lakini sasa tunamuona mtaani,” anasema Mkazi wa Manchali,

Joanita Kahambwa anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakilega lega katika malezi na kusabbaisha watoto kuzagaa ovyo kwenye vibanda vya video.

“Watoto hawachungwi, unakuta mtoto yupo kwenye kibanda cha video saa tatu usiku, mzazi hajui mtoto yuko wapi, ndio maana ukatili dhidi ya Watoto unaendelea,” anasema

Mratibu wa Dawati la Mtoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Sophia Swai anasema wamekuwa na changamoto kubwa ya kusimamia ukatili wa kijinsia kutokana na wazazi kutotoa ushirikiano na wengine kuogopa vitisho.

Anasema kuna kesi moja mzazi aliamua kusimama imara baada ya mtoto wake wa darasa la sita kupata ujauzito na kupewa vitisho.

Anasuimulia kwamba mtoto alipomtaja aliyempa ujauzito, akatumwa mgambo kwenda kumkamata kijana aliyetajwa, lakini kijana baada ya kuhojiwa alisema kwamba hayuko peke yake ‘katika kutembea na binti huyo.

Swai anasema kutokana na hilo baba mtu akashauri asuburi binti ajifungue ili vifanyike vipimo vya vinasaba (DNA) ili baba halisi wa mtoto apate kujulikana na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

Anasema wakati binti anajifungua wenzake walikuwa darasa la saba. “Baba wa binti akawa anapigiwa simu za vitisho, anaambiwa wewe mzee chukua hela wenzako wanakula hela tu shauri yako,” anasema Swai

Anasema kabla ya kwenda kwenye vipimo vya DNA binti alitoweka na mtoto na mpaka sasa hawajulikani walipo na inadhaniwa kwamba alitoroshwa ili kuua ushahidi.

“Mpaka leo binti hakujilikani alipo. Yule mzee kijijini wanamkejeli kiasi kwamba sasa anatamani ahame,” anasema na kuongeza kwamba huo ni mfano mbaya kwa familia zingine.

Swai anasema wananchi wana wajibu wa kuchukua matukio ya ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua. Mkazi wa Mpwayungu, Janeth Ndahani anasema baadhi ya wazazi wamekuwa hawaoni umuhimu wa elimu na hivyo kushindwa kuhamasisha watoto wafanye vizuri darasani ili wakifeli wakaolewe.

“Mtoto ananunuliwa kioo, wanja, rangi ya mdomo, nguo mpya na vingine na anaambiwa na mzazi kwamba usipofaulu nitakununulia vingi zaidi ya hivyo? Kwenye mazingira kama hayo mtoto ataona umuhimu wa shule kweli?” anahoji.

Anasema baadhi ya watoto wa kike hukataa kwenda shule wakidai wana mapepo ikiwa ni njama wao na wazazi wao.

“Hayo mapepo huwa ni wakati wa kuambiwa kwenda shule lakini wakiacha shule na kuolewa mapepo yanapotea… Lazima jamii iendelee kuelimishwa juu ya umuhimu wa elimu,” anasema.

Pia anasema kuna watoto wanaotoka vijiji vya jirani wanapanga nyumba karibu na maeneo ya shule na kwamba huwa na uhuru uliopitiliza. Mzazi mwingine, Sarah Chibwana anasema wazai wengi hawatimizi wajibu wao ipasavyo.

“Huku kwetu wazazi wengi huamia mashambani na kuwaacha watoto kujilea wenyewe na wakati mwingine wanaishiwa fedha za matumizi, watoto wanaingia kwenye makundi,” anasema Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mpwayungu, Jeremia William anasema kumekuwa na tabia ya wazazi kutaka kuoza watoto wao bila kujali kwamba bado wanasoma, jambo ambalo anasema linatakiwa kuendelea kufuatiliwa.

Anasema kuna wengine huamua kufanya vibaya mtihani wa kidato cha pili ili akifeli aende akaolewe. “Mzazi anaweza kuja shuleni kutoa taarifa kuwa mtoto wake wapotea, ukimuuliza kama alishakwenda kutoa taarifa kituo cha polisi anasema hapana, ukimuuliza kama mtendajhi ana taarifa anasema hapana, hapo ndio unajiuliza inawezekana vipi mtoto apotee lakini taarifa haijatolewa popote,” anasema.

Anasema hilo limekuwa ni tatizo kubwa katika jamii wazazi wanatorosha watoto ili wakaolewe. “Kuna mwanafunzi alitakiwa kuwa kidato cha nne, akapotea na aliporudi alikuwa na mtoto mkubwa tu.

Akaniona amajificha, siku moja nikamwambia uwe na amani tu. “Wazazi wengine huwa hawaoni kabisa umuhimu wa elimu. Tusiache hili la kuelimisha wananchi ili wabadilike, tuendelee kuwaelimisha umuhimu wa elimu kwa watoto bila kukata tamaa,” anasema.

Ofisa elimu kata ya Mpwayungu, Mussa Makalwe anasema elimu ni suluhisho la kuwatoa watoto katika mazingira kama hayo.

Anasema kesi nyingi za mimba za wanafunzi zinakosa ushahidi na hivyo wahusika kushindwa kuchukuliwa hatua.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpwayungu, Gabriel Hoya anasema taarifa nyingi za kesi za mimba huwa hana. “Bora nipewe taarifa ili nishindwe kutoa ushirikiano nilaumiwe.

Nitafuatiliaje jambo ambalo sina taarifa nalo, mimi huwa sipewi taarifa,” analalamika.

Edward Mgaya ambaye ni mzee wa kimila anasema wazazi wanatoa uhuru mkubwa sana kwa watoto wao na hawana muda na kukaa nao, hali inayochangia watoto kukosa maadili na hata kujihusisha na ngono mapema.

Mratibu wa WOWAP, Nasra Suleiman anasema jambo la msingi ni kuona jamii inashiriki ipasavyo katika kulinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto.

Anasema kila mtu kwa nafasi yake aone anafanya nini katika kupunguza tatizo mimba na ndoa za utotoni kwani lengo kubwa ni kuona watoto wengi wanahitimu masomo yao.

“Wanapoozwa au kupata mimba katika umri mdogo wanashindwa kutumiza ndoto zao,” anasema.

Anasema mradi huo ulioanza mwaka 2016, awamu nyingine ya utekelezaji inaendelea kupitia ufadhili wa The Foundation for Civil Society

Chanzo: habarileo.co.tz