Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hapi aagiza mnunuzi wa nyumba, mwanasheria NMB wakamatwe

48393 Pic+hapi

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Iringa kuwakamata mnunuzi wa nyumba ya marehemu, Peter Chang'a na mwanasheria wa Benki ya NMB  Iringa ili wakajibu madai ya kuuza na kununua nyumba hiyo.

Hapi ametoa agizo hilo jana Jumamosi Machi 23, 2019 baada ya mmiliki wa nyumba hiyo kwa sasa, Sauda Mlimakifi kulalamika katika mkutano wa mkuu huyo wa mkoa aliyekuwa akisikiliza kero za wananchi, uliofanyika kata ya Mwangata wilayani Iringa.

Sauda ambaye alikuwa mke wa Chang'a, mkazi wa Mwangata C, amesema mwaka 2007 alisikia nyumba yake imeuzwa na Benki ya NMB na kuamua kwenda kwenye benki hiyo kuhoji juu ya uuzwaji wa nyumba hiyo.

Akizungumza mbele ya Hapi, Sauda amesema baada ya kufika katika benki hiyo, alijibiwa na meneja wa NMB kuwa mume wake (marehemu) hajawahi kukopa kwa dhamana ya nyumba hiyo.

"Meneja alikiri kuwa nyumba hiyo ilipigwa mnada kimakosa na kuamua kunikutanisha na mnunuzi wa nyumba hiyo ambaye ni Niza  Gurdian. Baada ya kukutanishwa na mnunuzi huyo, NMB walimueleza kuwa nyumba hiyo amenunua kimakosa kwani  mtu aliyekopa kwao (NMB) ni Yunus Adam (mume wa sasa wa Sauda), si la mwenye nyumba hiyo,” amesema.

“Bali nyumba hiyo ina jina la mtu mwingine ambaye ni Peter Chang'a (mume wa zamani wa mlalamikaji) lakini mnunuzi alikataa kurudisha nyumba na kudai labda arudishiwe Sh15 milioni wakati mkopaji (Yunus) alikuwa anadaiwa Sh1 milioni.”

Sauda amesema kutokana na kipato chake duni, hakuwa na uwezo wa kumrudishia Sh15 milioni na tangu wakati huo walikaa kimya na kumuacha aendelee kuishi katika nyumba hiyo.

Amebainisha kuwa ilipofika Septemba 14, 2018 mama huyo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Riziki akitokea kampuni ya Majembe na kumueleza kuwa anatakiwa nyumbani kwake na baada kufika, alikuta askari wengi pamoja na Niza (mnunuzi wa nyumba) wakiwa tayari wamemtolea vitu vyake nje na kufunga nyumba.

“Tangu muda huo nimekuwa nikiishi nje ya nyumba yangu, nimefunga mahema naishi na watoto wangu hapo. Hivyo baada ya kusikia mkuu wa mkoa (Hapi) anawafuata wananchi na kusikiliza kero za ardhi nimejitokeza na kuelezea ili nipate haki yangu na watoto wangu kwa maana nyumba si yangu ni ya marehemu mume wangu na ni haki ya watoto.”

Akizungumzia sakata hilo, Adam amesema amekuwa akikopa NMB na alikuwa anaweka dhamana ya biashara yake na vitu vya ndani lakini alishangaa kusikia nyumba imepigwa mnada.

"Mimi sikuwahi kukopa NMB na kuweka dhamana ya nyumba nilikuwa nikikopa na kuweka dhamana ya biashara yangu na vitu vya ndani, meneja wa NMB aliyekuwepo kipindi hicho ana taarifa za mikopo yangu na dhamana,” amesema.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hapi ametoa amri ya kukamatwa kwa mnunuzi wa nyumba hiyo na mwanasheria wa NMB na kufikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya kuhojiwa.

Amesema hataki kuona wananchi wanyonge wanaonewa kama vile hawana haki ya kuishi ndani ya nchi yao na wengine kujiona ndio wenye haki ya kuishi na kufanya jambo lolote kwa vile tu wanatumia uwezo wao wa kifedha.

Amemhakikishia mama huyo kupata haki yake ya msingi kwa njia ya kisheria na si vinginevyo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz