Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hapi: Ndoto ya Magufuli yatimia

49722 HAPI+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema ametimiza ndoto ya Rais John Magufuli ya kuifanya Iringa kuwa kitovu cha utalii katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kukarabati majengo ya abiria ya Uwanja wa Ndege wa Nduli na kuweka jiwe la msingi ili ndege kubwa ziweze kutua.

Hapi alisema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi la ukarabati wa majengo ya kupumzikia abiria katika Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo mkoani hapa na kueleza kuwa dhamira ya Rais Magufuli ni kuiona Tanzania inafungua utalii wa Nyanda za Juu Kusini na kitovu chake kuwa Iringa.

Alisema ujenzi na ukarabati wa majengo hayo umegharimu Sh400 milioni ikiwa ni michango ya wadau kuhakikisha ndoto ya ndege kubwa kutua mkoani hapa inatimia ili watalii na wawekezaji waweze kufika kwa urahisi.

Hapi alisema alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Iringa kitu cha kwanza aliangalia ndoto ya Rais juu ya mkoa huo kwa kuiangalia mbuga ya Ruaha kwa sababu ndio pekee yenye simba wengi nchini.

“Mwaka jana siku ya Mei Mosi nikiwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni kabla sijaja Iringa Mheshimiwa Rais alikuja Iringa na kuzungumza na wananchi katika sikukuu ya wafanyakazi na kuahidi kuhakikisha ndege kubwa zinatua mkoani hapa ili kutanua uchumi kupitia utalii,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ndoto hiyo imeanza kutimia taratibu kutokana na ukarabati wa uwanja huo ili ndege kubwa ziweze kutua na kukarabati jengo la abiria ili abiria waweze kupata sehemu ya kupumzikia iliyo bora.

“Sasa tuna uhakika ndege kubwa zikianza kutua tutapata watalii wengi, wawekezaji wengi na uchumi wa Iringa utakuwa kupitia uwanja wa ndege kwani wawekezaji wengi hawana muda wa kupanda mabasi na watalii hawapendi kutumia muda mrefu barabarani badala ya mbugani,” alisema.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa Shirika la Ndege ATCL, Ladislaus Matindi alisema ndege kubwa ya ATCL ya kwanza itatua katika kiwanja hicho Aprili 29 mwaka huu “Zote hizi ni juhudi za mkuu wa mkoa pamoja na aliyekuwa meneja wa Uwanja wa Nduli, Hana kibopile.”

“Uwanja wa Iringa ulikuwa katika mpango wa miaka mitano, tulikuja na kuangalia tukaona haiwezekani lakini baada ya Hapi kuja ofisini na kuzungumza tuliona ni kitu kinachowezekana,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz