KATIKA kuhakikisha kiwango cha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari kinapanda katika Mkoa wa Dodoma, kila halmashauri imetakiwa kuweka mikakati na kuifuatilia kwa kina ikiwemo ya kuwashirikisha wazazi na wadau wa elimu wanafikia malengo ya kupandisha ufaulu kwa mkoa huo.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy, alibainisha hayo wakati akiwasilisha tamko la mkoa katika kikao cha wadau wa elimu mkoani Dodoma waliokutana kushirikishana mbinu katika kuboresha elimu na kiwango cha ufaulu mkoani humo.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, aliwataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kusimamia maelekezo hayo sambamba na kuwasimamia waratibu wa shule akiwasisitiza kuwa wabunifu katika kutekeleza tamko hilo.
“Tutakuwa tukikutana na kamati kutathmini nini kimefanyika Chemba na nini kimefanyika Kondoa ili kuhakikisha haya tunayokubaliana yanatekelezeka na mnapokutana na ugumu wowote tushirikishane mapema ili tufike tulipopataka,” alisema Dk Mahenge.
Naye Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuna haja ya kufanyika tathmini kwani viongozi wengi ngazi ya kata hawatekelezi majukumu yao, hivyo hawana budi kufuatiliwa kwa karibu ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.
Akijikita katika mikakati ya kuongeza ufaulu, Katibu Tawala, Kessy, alisema kila halmashauri lazima iwe na mikakati sambamba na kuipangia bajeti ili kupunguza kiwango cha kufeli kwa wanafunzi na kushughulikia vikwazo vyote vya watoto kushindwa kuzingatia masomo ili kuongeza ufaulu.
“Kila halmashauri kuwe na ufuatiliaji wa kina wa ufundishaji wa kila shule na kila mwalimu, mkuu wa wilaya asimamie wakurugenzi wake na mkurugenzi asimamie wakuu wa idara hadi ngazi za chini; tunataka ufaulu upande hapa tulipo ni aibu tupu,” alisema Maduka.
Alisema Dodoma sasa ni mkoa wa kisera na utawala hivyo, ni aibu kuona mkoa ukishika nafasi za chini katika kiwango cha ufaulu.
Alibainisha kuwa, wameweka mikakati mbalimbali baada ya miaka mitatu wawe nafasi ya 15 na mwaka 2025 kuwa namba chini ya 10 kitaifa.
“Tunataka halmashauri zetu ziondoke huko kwa sasa na kila halmashauri iwe chini ya 100 kitaifa ili kiwango cha kimkoa kipande; yote haya yatafanikiwa ufuatiliaji wa kina kila ngazi ukifanyika,” alisema.
Alisema kila halmashauri iweke utaratibu wa kuweka mikutano na wazazi ili kuwashirikisha katika mambo mbalimbali na siku hiyo itumike kusoma matokeo ya wanafunzi ili wazazi wajue nafasi za watoto wao ili wasaidie kuongeza hamasa na kuwasimamia watoto huku watoto nao pia, wakiongeza juhudi na kujituma katika masomo.
Katika tamko hilo, amezitaka halmashauri zenye shule na wanafunzi wanaozidi 800 kwa shule ya msingi na 500 kwa sekondari, kuanza kujiandaa kujenga shule nyingine au kujenga shule shikizi.
“Katika chumba kimoja cha darasa kwa shule za msingi, wasizidi wanafunzi 50 na kwa sekondari, wasizidi 40,” alisema.