Buchosa. Siku chache baada ya gazeti hili kuandika makala inayohusu adha ya vyoo visiwani, halmashauri ya wilaya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo ndani ya visiwa hivyo.
Watu wa visiwa 14 vya halmashauri hiyo wanajisaidia kwenye miamba pembezoni mwa Ziwa Victoria hali ambayo ni hatari kwa afya.
Mkurugezi wa halmashauri hiyo, Crispin Luanda alilieleza Mwananchi juzi kwamba wametenga Sh42 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyoo 14 vyenye matundu sita katika visiwa hivyo.
“Tunataka kuondoa wimbi la wakazi wa visiwani kujisaidia kwenye miamba pembezoni mwa ziwa Victoria, fedha tumeshazitenga na tunatarajia kuanza ujenzi huo haraka iwezekanavyo,” alisema Luanda
Alisema wamepanga kuanza ujenzi huo Februari na ujenzi huo utasimamiwa na halmashauri hiyo hadi kukamilika na kila choo kitagharimu Sh3 milioni.
Halmashauri hiyo ina kata 21, vijiji 82, vitongoji 410, kaya 54,624, visiwa 14 na idadi ya watu 435,555, hiyo ni kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasalazi Kisiwani, Masunga Kipolo alisema mpango huo utawasaidia kuacha kukimbizana na watu kujisaidia kwenye miamba kwa kuwa imekuwa kero kwenye visiwa hivyo.
Alisema watu wanaoishi visiwani jamii kubwa ni wavuvi hivyo wanatakiwa kudhibitiwa kutokana na ubishi wao hivyo wakijengewa choo itakuwa rahisi kuwabana ili waache tabia ya kujisaidia kwenye miamba.
Mmoja wa wakazi wa Kisiwa cha Zilagula, Amana Juma alisema mpango huo ulichelewa kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na jamii ya wavuvi wanaoishi kwenye maeneo hayo.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Buchosa Dk Ernest Chacha alisema mwaka 2015 wakazi wa visiwa hivyo 800 waliugua kipindupindu na kati yao 17 walipoteza maisha kutokana uchafuzi wa mazingira hivyo mpango huo utamaliza tatizo hilo.