Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri yasaidia wakulima wa muhogo

B87a66dad906d532a7e7bbb898068efc.jpeg Halmashauri yasaidia wakulima wa muhogo

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ZAIDI ya wakulima 400 wilayani Handeni mkoani Tanga wamehamasika kulima zao la muhogo baada ya kupatiwa mbegu bora na utaalamu wa jinsi ya kupanda.

Hayo yamesemwa na wakulima wakati waandishi wa habari walipotembelea mradi wa shamba darasa unaoendeshwa na Halmashauri ya wilaya ya Handeni Vijijini.

Walisema kuwa hapo awali walilima muhogo kwa ajili ya chakula na walikuwa hawapati tija ya kutosha.

Ruben Nkwe alisema kuwa walikuwa wanalima kimazoea na wakati mwingine hawakuwa wakipata mbegu bora hivyo kushindwa kufikia lengo.

Ahmed Mdoe alisema kuwa kwa elimu waliyoipata ekari moja wanapanda miche 4,096 na kutoa mihogo ambayo inaviwango vinavyohitajika na soko .

"Kupitia mafunzo haya sasa tumeanza kuona mwanga wa kunufaika katika kilimo hiki cha muhogo kwani mavuno yamekuwa mengi na zao hilo linauzika kwa urahisi sokoni," alibainisha Mdoe.

Hata hivyo, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni, William Makufwe alisema halmashauri imewapatia fedha ili waweze kulima kilimo chenye tija.

Alisema kuwa jumla ya wakulima 431 wamewapatia kiasi cha Sh bilioni 3.4 kwa ajili ya kulima zao hilo kwenye eneo lenye ekari 2,370 wilayani humo.

"Lengo letu ni kuuza zao hilo kimataifa na wakulima wetu waweze kupata fedha lakini na halmashauri nayo iweze kukusanya mapato yake kwa vizuri," alisema mkurugenzi huyo.

Aidha alisema kuwa zao hilo litakapokuwa tayari kuna kampuni ambayo itaweza kununua mihogo hiyo yote kwa ajili ya kuuza kwenye soko lake lililopo nchini China.

Tayari Tanzania imefanikiwa kuuza tani 1,000 za mihogo mikavu kwa nchi ya China, hivyo bado kunahitajika jitihada zaidi za kuongeza uzalishaji ili kuweza kuliteka soko hilo.

Chanzo: habarileo.co.tz