Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri ya Msalala yatoboa siri ya kuongoza kimapato ya ndani

81172 Msalala+pic Halmashauri ya Msalala yatoboa siri ya kuongoza kimapato ya ndani

Tue, 22 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Siku moja baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo kuitangaza halmashauri ya Msalala ya mkoani Shinyanga kuwa ya kwanza kitaifa kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani, uongozi wa halmashauri hiyo waeleza siri ya mafanikio.

Jana Jumatatu Oktoba 21, 2019  akizungumza na wanahabari Jijini Dodoma, Jafo aliitaja halmashauri hiyo kuwa ya kwanza baada ya kukusanya asilimia 52 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Msalala, Simon Berege alisema kutekeleza majukumu kama timu miongoni mwa watumishi ni siri mojawapo ya mafanikio iliyochangia kushika nafasi ya kwanza.

“Ukiona timu yetu ya mapato ikiwa kazini hujui ofisa ni yupi, ni kazi tu. Kwenye mapato sisi tunafanya kama timu, huwezi amini lakini ndiyo ukweli sisi hadi madiwani wetu, wote wanatusaidia kukusanya na kudhibiti,” alisema Berege.

Japo jingine lililosaidia ni maelekezo ya Rais wa Tanzania, John Magufuli aliyeagiza kuanzishwa kwa kituo cha kukusanyia dhahabu toka kwa wachimbaji wadogo wa  eneo la Kakola  ambalo limechangia kunyanyua mapato hayo tangu kianzishwe Agosti 2 mwaka huu.

“Dhahabu ya Sh25 bilioni imenunuliwa na halmashauri imepata kodi ya huduma ya zaidi ya Sh70 milioni, ambapo awali fedha hizi zilikuwa hazipatikani. Tumefanya vizuri kwenye udhibiti wa ushuru wa mazao hususan dengu hadi robo mwaka inamalizika zao hili lilitupatia Sh130milioni,” alisema

Pia Soma

Advertisement
Mbali na hilo, Berege alimshukuru Waziri wa Madini, Doto Biteko kwa maelekezo yake sambamba uongozi wa mkoa akiwa mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack na mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha kwa ushirikiano wao.

“Baada ya kutangazwa washindi mkuu wa mkoa wa wetu (Telack), ametupa pongezi na kutuambia tuongeze juhudi ili robo nyingine tuwe wa kwanza na tuendelee kuchapa kazi kama timu,” alisema Berege.

Chanzo: mwananchi.co.tz