HALMASHAURI ya Wilaya Madaba, mkoani Ruvuma imetoa Sh 87,000,000 sawa na asilimia 100 kama mikopo isiokuwa na riba kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye walemavu kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ulioishia Juni, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Shafi Mpenda alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa viongozi wa vikundi vya kijamii vilivyofanikiwa kusajiliwa kwa njia ya mfumo mpya wa mtandao.
Alisema mwaka wa fedha 2019/2020 halmashauri hiyo kupitia mapato yake ya ndani, ilitoa Sh 30,000,000, kati ya hizo vikundi 12 vya wanawake vilipata Sh 25,300,000, kikundi kimoja cha vijana Sh 3,000,000 na kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu Sh 2,000,000.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2020/2021, halmashauri hiyo iliweka lengo la kutoa mikopo ya Sh 74,000,000, hata hivyo imevuka lengo kwa kutoa Sh milioni 87, kati ya hizo wanawake walipata Sh 58,338,000, vijana Sh milioni 19 na walemavu Sh milioni 10.
Mpenda alisema hayo ni mafanikio makubwa kupatikana tangu Halmashauri ya Madaba ilipoanzishwa rasmi mwaka 2015 na kwamba wataendelea kuboresha kiwango cha mikopo kadri halmashauri itakavyofanya vizuri kwenye makusanyo ya ndani.
Aidha, alisema halmashauri hiyo imeanza kufanya utambuzi rasmi wa vikundi 123 vya kijamii vilivyosajiliwa kwa mfumo wa mtandao na utekelezaji wa maagizo ya serikali kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyotaka.
Mpenda alisema hatua hiyo imesaidia kuongeza mahusiano kati ya ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na wana vikundi ambao kupitia hafla hiyo watafahamu wapi pa kwenda wanapohitaji mikopo au huduma nyingine ambazo zinahitaji ushauri na msaada wa wataalam.
Alisema lengo la kukutana na vikundi hivyo ni kwa ajili ya kufahamiana, kutengeneza mkakati na utaratibu mzuri utakaosaidia kuboresha vikundi hivyo kupitia idara ya maendeleo ya jamii na namna wana vikundi wanavyoweza kupata elimu juu ya kuendesha vikundi vyao.
Alisema Halmashauri ya Wilaya Madaba itaendelea kutoa ushirikiano kwa wananchi ili vikundi vinavyoanzishwa na kuibuliwa viwe na tija na viwasaidie kuboresha maisha yao kupitia miradi na kuitumia ofisi ya Mkurugenzi na wataalam waliopo kupata huduma bora na kutoa taarifa pale wanapoona kuna changamoto katika uendeshaji wa vikundi vyao.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii Msaidizi wa halmashauri hiyo, Bashiru Mgwasa alisema jumla ya vikundi 114 vimesajiliwa, kati ya hivyo vya wanawake ni 48, vijana 16 na watu wa kundi maalum nane na mchanganyiko 42.
Mgwasa alisema jumla ya wanachama waliosajiliwa kupitia vikundi hivyo ni 1680, kati yao wanaume 443, wanawake 1237 na vikundi hivyo vinatoka katika vijiji 22 vilivyopo katika kata zote nane za Halmashauri ya Wilaya Madaba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Madaba, Theofanes Mlelwa alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aliitaka Idara ya Maendeleo ya Jamii kuendelea kuvitambua vikundi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na kutoa mikopo kwa wananchi hasa wenye mahitaji maalum ili waweze kujitegemea na kuondokana na umasikini.