Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri nchini Tanzania zatakiwa kuandaa takwimu za wakimbizi

Halmashauri nchini Tanzania zatakiwa kuandaa takwimu za wakimbizi

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk Philip Mpango amezitaka halmashauri kuandaa takwimu za wakimbizi katika maeneo yao kwa kubainisha mambo muhimu kama mahitaji yao na shughuli za kiuchumi.

Dk Mpango ameeleza hayo leo Alhamisi Novemba 28, 2019 jijini Dar es Salaam katika  maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika mwaka 2019  iliyowakutanisha watalaam wa masuala ya takwimu kutoka sehemu mbalimbali.

Amesema idadi ya wakimbizi Tanzania imepungua kutoka 521,282 mwaka 2017 hadi 337,005 mwaka 2018. Amesema kupungua huko kunatokana na kuimarika kwa hali ya usalama kwenye nchi zao.

"Hali ya usalama katika nchi nyingi iko shwari, Serikali inawahimiza wakimbizi kurejea makwao ili kuzijenga nchi zao,” amesema Dk Mpango na kuongeza kuwa mpaka sasa Tanzania imetoa uraia kwa wakimbizi zaidi ya 200,000.

Amesema takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR) zinaonyesha idadi ya wakimbizi duniani imeongezeka mara mbili zaidi kutoka milioni 43.3 mwaka 2009 hadi milioni 70.8 mwaka 2018.

Waziri huyo amesema ongezeko hilo limesababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo machafuko ya kisiasa, kuteswa, vita na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amebainisha ripoti hiyo ya UNHCR inaonyesha asilimia 67 ya wakimbizi duniani wanatoka katika nchi tano ambazo ni Syria, Afghanistan, Sudan Kusini, Myanmar na Somalia. Amesema nusu ya wakimbizi wote duniani ni watoto chini ya miaka 18.

Dk Mpango amezitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) na NBS kuendelea kushirikiana kuandaa takwimu zitakazoisaidia Serikali kufanya uamuzi.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema NBS imekuwa ikitumia takwimu za sensa kupata takwimu za wakimbizi. Amesema wameanza kuwatumia watakwimu wa halmashauri katika kuandaa takwimu halisi za wakimbizi.

Chanzo: mwananchi.co.tz