Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri Same yapewa miezi sita kuboresha masoko

Rgerhd Halmashauri Same yapewa miezi sita kuboresha masoko

Mon, 18 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni ametoa miezi sita kwa halmashauri ya wilaya hiyo, kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya masoko ili kupunguza kero kwa wafanyabiashara.

Amesema masoko hayo yasipoboreshwa yanaweza kusababisha ukusanyaji wa mapato kuwa mdogo, hivyo kutofikiwa kiwango kilichokusudiwa.

Mgeni ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Machi 18, 2024 alipotembelea na kukagua masoko likiwamo la Kwasakwasa mjini Same, alikosikiliza kero za wafanyabiashara.

"Leo nimetembelea masoko ya hapa mjini likiwamo la Kwasakwasa, nimepokea kero na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu changamoto zinazowakabili, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya masoko. Niwahakikishie wananchi, kero hizi tunaenda kuzitatua ndani ya muda mfupi," amesema na kuongeza:

"Maelekezo yangu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, ndani ya miezi sita nataka marekebisho kwenye masoko yote, tuanataka yaboreshwe ili wafanyabiashara wafanye biashara kwenye maeneo mazuri, yanayovutia wateja ili mapato yaweze kuongezeka."

Amesema, "Biashara zao zikiwa nzuri na sisi halmashauri tutapata mapato kutoka kwao ili kuendelea kukuza uchumi wa wilaya hii ya Same."

Mgeni amewataka wafanyabiashara kuwa mstari wa mbele kutunza mazingira ya masoko hayo na kuacha kutupa taka ovyo, kwa kuwa yapo maeneo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.

Mfanyabiashara katika soko la Kwasakwasa, Rebecca Mdee amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ubovu wa vibanda wanavyotumia ambavyo ni vya miti.

Amesema choo wanachokitumia kinahitaji kufanyiwa maboresho.

"Vibanda tunavyotumia hapa sokoni ni vibovu licha ya kwamba tunalipa ushuru wa soko. Tunaomba Serikali iangalie namna ya kutuboreshea, angalau vijengwe kwa mbao visiwe kama hivi vilivyo, maana upepo ukija hapa unabeba vibanda vyote," amesema Rebecca.

Salim Mwanga, kwa upande wake ameiomba Serikali kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili wafanye biashara yenye tija.

"Soko hili limejengwa kitambo kidogo, lakini miundombinu yake si ya kuridhisha, ukiangalia vibanda tunavyotumia si rafiki kabisa kwa mfanyabiashara," amesema.

Masoko mengine aliyoyatembelea ni ya Makanya, Hedaru na Mabilioni ambayo miundombinu yake inatajwa na wafanyabiashara wilayani humo kuwa si rafiki kwa shughuli zao.

Chanzo: Mwananchi