Halmashauri ya Igunga, inatarajia kukusanya jumla ya Sh39.7 bilioni huku mapato yake ya ndani yakiwa Sh4.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Akisoma rasimu ya bajeti, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Loyce Fumbu amesema kwa mapato ya ndani ni sawa na ongezeko la asilimia 16 ukilinganisha na mwaka wa fedha wa 2022/23 walipoweka Sh3.8 bilioni.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24, halmashauri inatarajia kupokea jumla ya Sh30.6 bilioni kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.
"Kwa kukusanya shilingi bilioni nne na milioni mia nne, ni sawa na ongezeko la asilimia kumi na sita,"amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elias Sambo amesema ili kufikia lengo la makusanyo hayo tayari wamezungumza na kuweka mikakati na watendaji wa kata na vijiji ili wafanye kazi kwa weledi mkubwa.
Amesema wanasisitiza matumizi ya mashine maalum za kukusanya mapato maarufu kama POS na kwamba wale watakaokwenda kinyume watashughulikiwa.
"Hatutakuwa na mzaha kwa wale watakaokaidi matumizi ya mashine hizo kwani pia tutawachukulia hatua za kisheria,"amesema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Bugota amewataka madiwani wote kutoa ushirikiano kwa watendaji ili wafikie lengo walilojiwekea la kukusanya kiwango hicho.
"Tutoe ushirikiano mkubwa kwa watendaji ili waweze kufanya kazi zao vizuri huku sisi pia tukiwa wasimamizi kwenye maeneo yetu," amesema.
Wajumbe wa kikao hicho kwa kauli moja wamepitisha rasimu hiyo ya bajeti ya kukusanya Sh39.7 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24.