Mkoa wa Dodoma umekusanya mapato ya zaidi ya Sh bilioni 21.955 ambayo ni sawa na asilimia 35 ya makadirio ya halmashauri saba ya kukusanya zaidi ya Sh bilioni 64.069 kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu. Alisema mkoa unaendelea kufanya jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kupanua shughuli za maendeleo ambapo hadi kufikia Novemba mwaka huu umekusanya Sh milioni 21.9, sawa na asilimia 35 ya makisio ya kukusanya Sh milioni 64 kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Kwa upande wa utengaji wa fedha za maendeleo, Mtaka alisema kwa mwaka wa fedha 2020/21, Sh milioni 27.4 zilitengwa na kutolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye halmashauri zote saba.
“Aidha, katika bajeti ya 2021/22 makisio ya mapato ni shilingi 64,069,966,000 ambapo shilingi 42, 339, 858,025 zinatarajiwa kutengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa kipindi cha Julai hadi Novemba mwaka huu, shilingi 9,715,664,957 zilitolewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo,” alisema.
Aliongeza: “Hivyo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, shilingi 37,131,924,765 zilitolewa na halmashauri zote kwa ajili ya shughuli za maendeleo.” Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Mkoa wa Dodoma uliidhinishiwa Sh milioni 314.7 ambapo kati ya hizo Sh 128.4 ni fedha za maendeleo huku Sh milioni 69.6 zikiwa ni fedha za ndani na Sh milioni 58. 7 fedha za nje.
Hadi kufikia Novemba mwaka huu, fedha zilizopokelewa ni Sh milioni 115, sawa na asilimia 33.66 ya bajeti iliyoidhinishwa ambapo Sh milioni 95.5 zimetumika. Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango wa maendeleo ya taifa na mapambano dhidi ya Covid-19 ambapo Mkoa wa Dodoma ulipatiwa Sh milioni 17.6, hivyo kufanya bajeti ya mkoa kuwa Sh milioni 359.3.
“Fedha zilizotengwa zimewezesha kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwamo ya madarasa ya shule za msingi na sekondari, ujenzi wa maabara na matundu ya vyoo, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, majengo ya utawala, utengenezaji wa madawati, uimarishaji na ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi ya kimkakati,” alieleza.
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, Mtaka alisema mpaka Novemba 2021, mikopo ya Sh bilioni 5.81 ilitolewa, sawa na asilimia 97 ya lengo la kutoka mikopo yenye thamani ya Sh bilioni sita huku vikundi 461 vikinufaika na mikopo hiyo, vikihusisha vikundi 282 vya wanawake, 136 vya vijana na 43 vya watu wenye ulemavu.
Kuhusu mapato ya Mamlaka ya Mapato (TRA), Mtaka alisema hadi kufika Novemba 30, mwaka huu imekusanya Sh bilioni 164.6, sawa na asilimia 91 ya malengo ya kukusanya Sh bilioni 180.58 huku ikisajili walipakodi wapya 3,315 hivyo kufanya mkoa kuwa na walipakodi 19,556.