Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Halmashauri 79 zatoa mikopo wanawake, vijana kwa 100%

734e1a81492172c8cd528d6c18e71630 Halmashauri 79 zatoa mikopo wanawake, vijana kwa 100%

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TANGU kuanza kutumika kwa Sheria ya Utoaji wa Mikopo kwa Vikundi mbalimbali vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika mwaka wa fedha 2018/19 na 2019/20, halmashauri 79 zimetoa mikopo kwa asilimia 100 na halmashauri 54 zimetekeleza kwa asilimia zaidi ya 85.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni Dodoma jana na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Asia Halanga (CCM).

Halanga alitaka kujua ni halmashauri ngapi nchini zimetekeleza kwa asilimia 100 sheria hiyo ya utoaji mikopo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani kwa makundi ya vijana, akina mama na watu wenye mahitaji maalumu.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, hali ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri nchini imeimarika.

Alisema kazi hiyo imeimarika hasa, baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 yaliyofanyika Julai, 2018 kwa kuongeza Kifungu cha 37A kuhusu mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Tangu kuanza kutumika kwa sheria hii katika mwaka wa fedha 2018/19 na 2019/20, halmashauri 79 zimetoa mikopo kwa asilimia 100 na halmashauri 54 zimetekeleza kwa asilimia zaidi ya 85,”alisema.

Dugange alisema utekelezaji wa sheria hiyo, umewezesha kuongezeka kwa mikopo inayotolewa na halmashauri nchini, ikilinganishwa na kipindi kabla ya kufanya marekebisho ya sheria.

Katika mwaka wa fedha 2017/18 (kabla ya marekebisho ya Sheria) Sh bilioni 26.1 zilitolewa, mwaka wa fedha 2018/19 baada ya marekebisho ya Sheria Sh bilioni 42.06 zilitolewa na mwaka wa fedha 2019/20 jumla ya mikopo iliyotolewa ilikuwa ni Sh bilioni 40.7.

Kwa mujibu wa Kifungu Namba 24(2) cha kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019, inawataka wakurugenzi kusimamia utelekelezaji wa kanuni hiyo.

“Mkurugenzi ambaye atashindwa kusimamia utekelezaji wa kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu inaweza kwa kadri itakavyoona inafaa, kumchukulia hatua za kinidhamu,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz