Mabasi ya abiria, magari madogo, bajaji na pikipiki yameanza kupita katika baadhi ya maeneo ya barabara ya mabasi yaendayo haraka 'mwendokasi' inayoanzia Kariakoo hadi Mbagala mkoani Dar es Salaam, baada ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa kumtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuratibu zoezi hilo kwa kipindi ambacho barabara hizo hazijaanza kutumika na mabasi yaendayo haraka.
Hali hiyo imeonekana mapema hii leo ikiwa ni saa chache baada ya suala hilo kutolewa maelekezo ya kuwawezesha wananchi kutumia miundombinu ya mabasi ya mwendokasi iliyokamilika kujengwa na haijaanza kutumiwa, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam hasa majira ya asubuhi na jioni.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwa katika ziara yake ya usiku ya kukagua miradi ya maendeleo alitoa maelekezo kwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam, ifikapo saa mbili asubuhi ya leo magari madogo na mabasi ya abiria yawe yameanza kutumia barabara hizo mpaka mradi huo utakapoanza.