Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, Cleofas Waane aliyekuwa akisikiliza kesi ya kijana Elpidius Edward (22) anayedaiwa kuvamia na kufanya uharibifu katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Jimbo la Geita, amejitoa kwenye kesi hiyo kutokana na mgongano wa kimaslahi.
Kesi hiyo ambayo jana Aprili 3, 2023 ilikuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali imeshindikana baada ya hakimu Waane kujitoa kutokana na yeye kuwa muumini wa Kanisa Katoliki.
Kufuatia kujitoa kwa hakimu Waane,hakimu mkazi Mfawidhi mwandamizi Samwel Maweda ameipanga kesi hiyo kwenda kwa hakimu Johari Kijuwile aliyeiahirisha hadi Aprili 12,2023 itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.
Kesi hiyo namba 62 ya mwaka 2023 ilifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 6, 2023 na kusomewa mashtaka mawili ikiwemo la kuvunja na kuingia kwenye jengo la Kanisa kinyume na kifungu namba 261(1) na(2) cha sheria ya kanuni ya adhabu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Februari 26, 2023 katika Kanisa Katoliki Jimbo la Geita mshtakiwa alivunja na kuingia kwenye Kanisa akiwa na dhumuni la kufanya kosa na kuharibu mali.
Katika shtaka la pili mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa kosa la uharibifu wa mali kinyume na kifungu namba 326 kifungu kidogo cha kwanza cha sheria na kanuni ya adhabu na kusababisha uharibifu wa mali za Kanisa zenye thamani ya Sh48.2 milioni.
Mtuhumiwa huyo bado yuko rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakaokuwa na fedha taslimu Sh24.1 milioni au kuwa na hati ya ardhi yenye thamani ya fedha hizo.
Tukio la uvamizi Kanisa Kuu Jimbo la Geita lilitokea usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26,2023 ulisababisha kanisa kufungwa kwa siku 20 kuanzia Februari 27 hadi Machi 18, 2023 lilipofunguliwa kwa kufanyiwa ibada maalum ya kulitakatifuza.