Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Habibu: Risasi imekatisha ndoto yangu katika elimu

35364 Pic+risasi Habibu: Risasi imekatisha ndoto yangu katika elimu

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ulikuwa mwezi wa Ramadhani, Julai 2014. Na ilikuwa imebaki miezi miwili tu Habibu Amiri (19) afanye mitihani ya kumaliza darasa la saba siku alipopigwa risasi iliyomwacha na ulemavu wa kudumu.

Saa tano asubuhi wakati Habibu (pichani), aliyekuwa akisoma katika Shule ya Msingi Zeba, wilayani Lushoto, Tanga, alipotumwa na baba yake sokoni kununua mboga na vyakula vingine kwa ajili ya futari hakujua masahibu ambayo yangempata muda mfupi uliofuata.

Wakati akirudi nyumbani, jirani na eneo la Kiwanda cha Chai cha Mponde, ghafla alihisi amepigwa na kitu kigumu kwenye makalio. Alianguka huku damu zikimtoka kwa wingi.

“Nilipoanguka haukupita muda watu waliokuwa karibu walikuja wakanipakia kwenye bodaboda na wakanikimbiza Zahanati ya Mponde kupatiwa huduma ya kwanza kwa sababu nilikuwa navuja damu nyingi na maumivu yalikuwa makali,” anasema Habibu, mkazi wa Kweminyasa, Kata ya Mponde huko Bumbuli, Tanga.

Habibu hatausahau mgogoro kati ya wakulima wa chai katika skimu tano zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli na mwekezaji aliyekuwa akiendesha Kiwanda cha Chai Mponde uliozaa vurugu zilizomsababishia ulemavu. Alipigwa risasi wakati Jeshi la Polisi likiwatawanya mamia ya wananchi waliojazana eneo la kiwandani hapo kushinikiza kiwanda kifungwe kwa muda na mwekezaji aondolewe.

Kwa miaka mitatu mfululizo baada ya kupigwa risasi, kijana huyo alikuwa akilazimika kujisaidia kwa kutumia mipira iliyoingizwa tumboni.

Kijana huyo wa tatu katika familia ya watoto watano ya Amiri Omari (55) hakuweza kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutokana na kuuguza majeraha.

Wakati akipatiwa huduma ya kwanza katika zahanati, baba yake aliingia huku akitokwa machozi baada ya kuelezwa kuwa hali ya mtoto wake ilikuwa mbaya. Alijiuliza ilikuwaje mtoto aliyemtuma sokoni amelazwa katika zahanati?

“Nilienda nyumbani kwa rafiki yangu anayeitwa Jerry, anayekaa karibu na zahanati nikamuomba gari yake na bila hiyana naye akalitoa gari hilo, lakini halina mafuta ya kufika Lushoto,” alisema Omari.

Zilihitajika Sh50,000 za kununua mafuta yatakayoweza kuwafikisha Lushoto ambazo hakuwanazo. Jerry alitoa pia fedha hizo.

“Baada ya kupata gari nilikwenda kumchukua mwanangu na kumkimbiza mpaka hospitali ya Lushoto na baada ya vipimo walituambia kuwa hali yake ni mbaya hivyo akimbizwe KCMC kwa matibabu zaidi.

“Nilikuwa nikimuangalia mwanangu machozi yananitoka maana nilikuwa najua hawezi kupona tena, niliwaza sana maana mke wangu alikuwa ana siku tatu tu tangu ajifungue halafu mfukoni sina pesa.”

Alisema baada ya kufika hospitalini hapo alifanyiwa vipimo na madaktari wakaamua afanyiwe operesheni iliyochukua saa 48.

Baada ya upasuaji Omari alisema alitakiwa kulipa Sh1 milioni. “Nikaanza kuwaza na kuzunguka huku mawazo yakinizonga kwa sababu sikuwa na fedha mkononi. Ilibidi nirudi nyumbani na kuuza ng’ombe na shamba moja ili niweze kwenda kulipia gharama za matibabu,” anasema.

Alirudi hospitali na kulipa mgonjwa akaruhusiwa kurudi nyumbani.

Anasema waliporudi Bumbuli fedha ziliwaishia na wakawa hawana uwezo wa kununua pampasi. Ilibidi kuanza kutumia mifuko ya rambo kupokea uchafu.

Ilipofika tarehe ya kurudi KCMC, Omari hakuwa na fedha. Ilimbidi amtafute Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye alimsaidia Sh1 milioni ambazo walitakiwa kulipa kwenye upasuaji wa pili. Omari anasema fedha hizo ziliokoa maisha ya kijana wake.

“Kweli Mungu yupo. Hali aliyokuwa nayo Habibu sikutegemea kumwona akiwa hai leo. Tumshukuru Mungu na wote waliomsaidia,” alisema mmoja wa vijana ambao walimpeleka hospitali, Mussa Shehiza.

Habibu anasema bado anakumbuka jinsi alivyoshindwa kufanya mtihani kutokana na maumivu.

“Ndoto zangu za kujiendeleza kielimu zinafifia lakini bado naamini inawezekana kuzifufua na kuendelea na masomo. Naiomba Serikali inasaidie kutimiza ndoto yangu,” alisema kijana huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz