Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Habari za vijijini na siasa za mijni

33498 Pic+vijijini Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watu wengi na hasa wanasiasa wamekuwa wakilalamika kwamba waandishi wa habari wanakazania kuandika mambo ya mijini na kashfa nyingine za Serikali huku wakiacha habari nyingi za vijijini. Kiasi fulani, malalamishi haya ni ya msingi tukizingatia kwamba watu wengi wanaishi vijijini. Na vijiji vyetu vina matatizo mengi ambayo kama yangeibuliwa kwenye vyombo vya habari, labda yangetafutiwa ufumbuzi. Tumeshuhudia sakata la korosho ambalo tukitaka kuwa wa kweli bado halijapatiwa ufumbuzi wenye kuleta tija kwa mkulima. Kahawa, pia bado ni kitendawili, wakati nchi jirani bei iko juu sana, kwetu inashuka! Wakati soko la kahawa duniani ni lilelile. Kinachotokea hapa ni upole wa njiwa na ujanja wa nyoka. Tukiandika habari hizi za vijijini juu ya wakulima na mazao yao, wabunge wetu watapona? Wananchi wakiruhusiwa kupiga kura zao za siri, chini ya tume huru ya uchaguzi, ni wangapi watapona tukiyaandika ya vijijini?

Tunayaandika ya mijini na kuendeleza siasa za mijini kwa vile wanasiasa wote wako mijini. Vijijini ni wakati wa kampeni na kutafuta kura. Baada ya hapo siasa zote zinahamia mijini. Huu ni ukweli ambao haupingiki hata ukiangalia miradi mikubwa yote inaelekea mijini.

Malalamishi haya kwamba unaandika ya mijini na kusahau ya vijijini kwa upande wa wanasiasa yana utata: Je, tukiandika ya vijijini wanasiasa hawa, hasa wabunge wetu watapona? Asilimia kubwa ya wabunge wetu wanaishi Dar es Salaam. Kwa mfano mkoa wangu wa Kagera, ukimtoa aliyekuwa mbunge wa Biharamulo, Phares Kabuye (TLP) ambaye aliishi kijijini wabunge wengine wote wanaishi Dar es Salaam. Wanaishi vijijini wakati wa kampeni za uchaguzi na labda mara mojamoja wakati wa Christmas na mwaka mpya. Ninapoandika makala hii, tunapigana vikumbo kwenye safari za sikukuu za kufunga mwaka. Huu ni wakati wao wa kupitapita na kusalimia, lakini muda mwingi wanaishi Dar es Salaam. Sikatai ukweli kwamba wana mawasiliano na majimbo yao na wakati mwingine wanayatembelea. Hata hivyo, hii haitoshi kwa njia moja ama nyingine hawana nafasi ya kuyaishi na kuyagusa maisha ya wananchi.

Sekondari za kata zimebatizwa jina la yeboyebo. Jina ambalo linatilia shaka ubora wa shule hizi. Kusema ukweli watu wameitikia kuzijenga sekondari hizi za kata. Pamoja na kusukumana kutoa michango sekondari hizi sasa zipo na wanafunzi wanasoma. Jambo la kushangaza na kusikitisha ni kwamba walimu wanaofundisha sekondari hizi hawalipwi kwa wakati! Wanafundisha kwa matumaini kwamba watalipwa. Wengi wa walimu hawa ni wale waliokuwa wanafundisha zamani na wakastaafu. Hivyo wamekuwa na mkataba na serikali kufundisha sekondari za Kata. Lakini, pia tukumbuke kwamba tunapotaka kuijenga Tanzania ya viwanda, ni lazima kuboresha elimu yetu. Ni lazima kuwa na walimu wazuri na mfumo mzuri wa kuwafundisha watoto wetu. Ni sawa kujenga miradi mikubwa ya barabara, umeme na viwanda. Bila kuwa na mfumo mzuri na shule nzuri zenye walimu wazuri ni kazi bure.

Habari za vijijini ndio hizo, tunaweka nguvu kubwa kuiendeleza miji yetu na kuweka nguvu kidogo sana kuviendeleza vijiji vyetu. Tukitaka mabadiliko ya msingi ya kulijenga taifa letu na kuukuza uchumi, ni lazima tukazanie maendeleo ya vijijini. Watanzania wengi wanaishi vijijini na idadi kubwa ya watu ni mtaji wa maendeleo.



Chanzo: mwananchi.co.tz