Moshi. Wakati Serikali ikijitahidi kudhibiti ukwepaji wa kodi, imebainika kuwa baadhi ya watu katika mji wa Moshi, wanapokea watalii na kuwalaza katika nyumba za wageni ambazo hazijasajiliwa kibiashara.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa watalii hao hulazwa katika nyumba hizo ambazo hazina alama yoyote kuonyesha zinatoa huduma hiyo, na kutozwa kati ya dola 15 na 30 za Kimarekani kwa siku.
Fedha hizo ambazo zina thamani ya kati ya Sh34,000 na Sh66,000 za Kitanzania, hujumuisha kifungua kinywa, chakula cha mchana na jioni na wakati mwingine hupikiwa wali na maharage kwa Sh1,500 kwa sahani.
“Kwa wenzetu huko nje biashara hii inafanyika kihalali, lakini hapa Moshi sehemu kubwa inafanyika illegally (kinyume cha sheria). Hakuna kibao chochote maeneo hayo,” alisema mmoja wa watu waliozungumza na Mwananchi.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa sehemu kubwa ya wanaoendesha biashara hiyo ni Watanzania walioolewa na kuoa raia wa kigeni ama ambao waliwahi kuishi nje ya nchi na kujenga mtandao mkubwa.
Watu tofauti waliongea na Mwananchi wametaja maeneo ambayo yamekithiri kwa biashara hiyo kuwa ni kata za Rau, Mfumuni, Soweto na eneo la Shanty Town lililopo kata ya Kilimanjaro ambalo lina raia wengi wa kigeni.
Pia Soma
- Bongo movie, Swahilflix kumleta Will Smith Tanzania
- Rais Magufuli asisitiza bei elekezi zao la pamba ni Sh1,200
- NEC kuanza uboreshaji wa Daftari, Kihamia atoa mwongozo
- TCU yavifungulia vyuo vilivyofungiwa kudahili
“Kwa wale ambao wanamiliki hizo nyumba na hawana leseni za Tala (ya Serikali) kuhudumia watalii, huwa wananunua vocha kwa kati ya Sh50,000 na Sh100,000 kwa kila mtalii.”
Wadau wa utalii wafunguka
Mawakala wa utalii waliohojiwa na Mwananchi jana, walisema wanafahamu biashara hiyo bubu na kutaka mamlaka kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo ili kuinua mapato ya nchi.
Mmoja wa mawakala ambaye pia hakutaka jina lake litajwe, alisema nyumba hizo hazina leseni za kulaza wageni, wamiliki hawalipi kodi ya mapato wala kodi ya huduma (service levy) inayotozwa na halmashari.
“Unazungumzia hizo guest bubu (nyumba za kulala wageni) za watalii? Mbona ziko nyingi tu. Nenda kule Soweto, nenda Rau zipo. Serikali iitishe kikao cha wadau wa utalii tuyaseme haya,” alisema.
Mkurugenzi wa Hoteli ya Leopard, Priscus Tarimo alisema suala hilo lisipodhibitiwa, litaharibu uchumi wa nchi kama ilivyotokea huko Malindi nchini Kenya kwa wamiliki wa nyumba kama hizo ambao ni raia wa Italia.
“Mimi pia ni diwani wa Kata ya Kilimanjaro na tuliwahi kuzibaini nyumba sita za aina hii tukapambana nazo sana hadi zikaingia kwenye mfumo rasmi wa kulipa mapato ya Serikali,” alidai.
“Hili suala ndio liliharibu uchumi wa Malindi kama watu wanajua vizuri. Wataliano walinunua nyumba halafu wanamuacha mlinzi na mpishi tu na wao wanarudi kwao wanazitangaza,” aliongeza.
“Wakiwa huko wanazitangaza hizo nyumba kwenye mitandano kama Airbnb wanapata wageni na walikuwa wanakwenda Malindi (Kenya) wanapokelewa kama wageni wa familia kumbe sio.”
Tarimo alisema wamiliki walioko Italia humtumia mpishi na mlinzi matumizi yote muhimu ikiwamo chakula na vinywaji na kuwataka wawatembeze maeneo ya vivutio vya pwani.
“Wenyeji wanapoona ni wazungu wanajua labda ni wageni tu wa wamiliki wa hizo nyumba kumbe ni watalii. Polepole mapato ya Serikali yakaanza kushuka. Hiki ndio kimeanza kutokea hapa kwetu,” alisema.
Lakini mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema ndio kwanza anasikia kuhusu nyumba hizo.
“Lakini ninashangaa kama haya yanatokea huko na madiwani na viongozi wa mitaa wapo na kwanini wasiyabaini haya? Nakushukuru sana, nalifanyia kazi,”alisema.
Kwa mujibu wa Mwandezi, halmashauri inapaswa kutoza kodi ya huduma kwa kila kitanda ambacho mgeni amelala na kwamba watafanya utafiti kubaini nyumba hizo zilipo.
Alisema ndani ya kata kuna kamati za ulinzi na usalama, hivyo wanapaswa kuwa makini na wageni wanaoingia.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi naye alisema hakuwa na taarifa hizo na akawaomba wenye taarifa hizo waisaidie mamlaka ili ichukue hatua.