Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Giza lasababisha kusitisha shughuli ya uokoaji wa aliyefukiwa kifusi, jiwe

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Mkuu wa wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza,  Dk Philisi Nyimbi amelazimika kusitisha shughuli za uokoaji wa Ndalawa Ndobo mkazi wa mtaa wa Tambukareli kata ya Butimba anayedaiwa kufariki dunia baada ya kufukiwa na udongo na baadaye kuangukiwa na jiwe alipokuwa akichimba udongo wa kutengenezea majiko ya mkaa.

Dk Nyimbi ambaye pia mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alisema jana jioni kuwa, wamefanikiwa kuondoa jiwe lakini kazi ya kuondoa kifusi itaendelea leo kutokana na usiku kuingia.

Udongo huo unachimbwa katikati ya mawe katika eneo la milima ya Tambukareli jijini Mwanza.

“Shughuli ya ukoaji itaendelea kesho (leo) asubuhi lakini jiwe kubwa limeondolewa hivyo kazi kubwa iliyobaki ni kuondoa kifusi cha udongo kazi itakayofanyika kesho (leo).” alisema Dk Nyimbi

 

Awali, Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Jumanne Muliro akizungumza na Mwananchi jana alisema juhudi za uokoaji zinaendelea.

 

“Mtambo maalum tayari umepelekwa eneo la tukio kusaidia kuondoa udongo na mawe kufanikisha uokoaji,” amesema Kamanda Muliro.

Diwani wa Butimba, John Pambalu amesema kabla ya kuangukiwa na udongo na kukandamizwa na jiwe kuanzia kifuani, Ndobo na mkewe ambaye hakumtaja jina walikuwa wakichimba udongo kwa ajili ya biashara yao ya kutengeneza majiko.

“Kwa mujibu wa maelezo ya wakazi wa eneo la tukio, Ndobo na mkewe hufanya kazi ya kuchimba na kuuza udongo kwa ajili ya kutengeneza majiko ya mkaa na kabla ya tukio walikuwa wote,” alisema Pambalu

Alisema baada ya kutoka ndani ya shimo alimokuwapo mumewe, mke wa Ndobo alishangaa kuona mume wake amechelewa kutoka ndipo alipochungulia na kubaini ameangukiwa na udongo na kuita watu kumnasua.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz