Geita. Chanjo ya ugonjwa wa Surua, Rubella na Polio iliyokuwa itolewe mkoani Geita nchini Tanzania kuanzia kesho Alhamisi Septemba 26 hadi 30, 2019 kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano imeahirishwa kutokana na maandalizi kutokamilika.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Jumatano Septemba 25, 2019 mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema shughuli hiyo iliyokuwa ianze kesho limesogezwa mbele hadi Oktoba 15 hadi 19, 2019.
Amesema shughuli hiyo itawahusisha watoto zaidi ya 600, 000 wa mkoa huo ambapo watoto zaidi ya 413,000 wenye umri wa miezi tisa hadi miezi 59 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya surua na Rubela huku watoto 171,000 wenye umri wa miezi 18 hadi 42 watapatiwa chanjo ya sindano ya polio.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa maeneo 388 yametengwa kwa ajili ya kutolea chanjo na kwamba chanjo hiyo ni bure hivyo ni vema wazazi na walezi wakawapeleka watoto wao ili kuwakinga na magonjwa yanayosababishwa na virusi vinavyoeneza magonjwa hayo.
Mganga mkuu wa mkoa huo, Japhet Simeo amesema shughuli ya kutoa chanjo imesogezwa mbele ili kukamilisha maandalizi ikiwa ni pamoja na kuhakiki maeneo yatakayotolea chanjo, kusambaza chanjo kufika kwenye maeneo yaliyoainishwa pamoja na kutoa mafunzo kwa watoa huduma.