Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita wavutana mkoa mpya wa Chato

459aecdce8071428c3fb7441faf2eddc.png Geita wavutana mkoa mpya wa Chato

Sat, 29 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VUTA nikuvute imeibuka kwenye kikao cha Baraza la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Geita kuhusiana na uanzishwaji wa mkoa wa mpya wa Chato.

Mvutano ulikuwa kwenye maeneo ya hifadhi ya Rubondo na Wilaya ya Busanda.

Katika kikao hicho kilichofanyika juzi, baadhi ya wajumbe waliomba hifadhi ya Rubondo na jimbo la Busanda kuwa upande wa mkoa mpya wa Chato huku wengine wakipendekeza maeneo hayo mawili yabakie kuwa mkoa wa Geita kutokana na sababu za kijiografia.

Katika taarifa yake juu ya mchakato wa kuanzishwa mkoa mpya wa Chato, Kaimu Mkurugenzi wa Mtendaji wa Wilaya ya Geita, Edith Mpinzile alisema jimbo la Busanda ambayo ni wilaya tarajiwa imependekezwa kubakia Geita badala ya Chato kutokana na sababu za kijiografia.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa, kwa kuangalia sababu za kiuchumi ni vyema kisiwa cha Rubondo kikabakia mkoa wa Geita badala ya kupelekwa Chato kwani kimekuwa ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato kwa mkoa wa Geita.

Mbali na hayo, Mpinzile alieleza kuwa mkoa mpya tarajiwa wa Chato una hifadhi nyingi na mapori mengi ya misitu yanayoweza kutumika kama vyanzo vya utalii hivyo itakuwa vyema iwapo Rubondo itabakia Geita kuufanya mkoa kuendelea kuwa na chanzo cha utalii.

Diwani wa Kata ya Nkome, Masumbuko Nsembe alisema alisema hifadhi ya kisiwa cha Rubondo ni vyema ikabakia halmashauri ya wilaya na mkoa wa Geita kwani imekuwa ni moja ya vyanzo vikubwa vya mapato mkoani hapa.

Diwani wa Kata ya Rudete wilaya ya Geita jimbo la Busanda Sebastian Mullando, alisema wakati mchakato wa kuundwa mkoa wa Chato ukiendelea ni lazima pia suala la jimbo la Busanda kuwa wilaya liwekewe mkazo kwa sababu vigezo vyote vimetimia.

Kuhusu mji mdogo wa Katoro ambao umekuwa ni kituo kikuu cha kibiashara wilayani Geita, alipendekeza ni vyema mchakato wa kuihamisha Katoro kwenda Mkoa mpya wa Chato usitishwe kutokana na ukaribu kutoka Geita na umbali kwenda makao makuu Chato.

Diwani wa Viti Maalumu Halamashauri ya Wilaya ya Geita, Stefania Benjamini alisema haoni sababu ya kisiwa cha Rubondo na wilaya ya Rubondo kupelekwa mkoa mpya wa Chato kwani sababu za kijiografia zinayafanya maeneo haya kuwa karibu kupata huduma karibu zaidi na Geita na siyo Chato.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mwalimu Fadhili Juma akizungumzia mvutano huo alishauri ni vyema hifadhi ya Rubondo ibakie wilaya ya Chato kwa sababu za kiusalama lakini jimbo la Busanda ambalo linatarajiwa kuwa wilaya ni vyema ibakie mkoa wa Geita ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wake.

Chanzo: www.habarileo.co.tz