Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Geita kutengeneza magari ya umeme

2c609eb926a760fe97502a3a40998d71 Geita kutengeneza magari ya umeme

Fri, 25 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema kesho wataingia mkataba na kampuni moja ya kutengeneza magari ya umeme mkoani humo.

Aliyasema hayo jana wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Fursa za Uwekezaji na Biashara mkoani Geita uliofanywa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila.

Gabriel alisema mradi huo wa magari ya umeme ni uwekezaji muhimu katika mkoa ambao unakua kwa kasi na kuwa kitovu cha biashara ya madini na uwekezaji wa aina mbalimbali.

“Ndani ya miezi mitatu ijayo, magari mawili yatakuwa tayari yamekamilika na yatakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilometa 100 bila kuyachaji tena, hivyo kwa mtu ambaye atakuwa anasafiri kwa kilometa 50 atakuwa na uhakika wa kutolichaji gari lake kila siku,”alisema.

Alisema hayo ni mafanikio yanayochangiwa na biashara ya madini, hivyo sekta hiyo haipaswi kuchezewa na wachimbaji wadogo wanaweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amezitaka kampuni nyingine kubwa zinazochimba dhahabu mkoani Geita kuwajibika kwa jamii kama zinavyofanya kampuni zingine ikiwemo Kampuni ya Dhahabu ya Geita (GGM).

Alisema kampuni hizo licha ya kupata faida ya mabilioni ya fedha lakini zimekuwa haziwajibiki kwa maendeleo ya kijamii ya wana Geita.

“Hatuoni shida kuvunja mikataba kwa maslahi mapana ya Watanzania, tunataka tunufaike katika usawa, haiwezekani Watanzania wabaki kuwa watazamaji tu huku rasilimali zao zikiondoka bila kuwanufaisha," alisema.

Kuhusu suala la ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini, alisema licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya sheria ya madini, lakini bado idadi ya Watanzania waliopata fursa ya kufanya biashara na kampuni kubwa za madini ni ndogo kwa asilimia 20 hadi 30 badala ya kuwa asilimia 80.

Alizitaka kampuni ambazo zilikuwa na mikataba kabla ya mabadiliko ya sheria kuhakikisha mikataba yao inapofikia ukomo na watakapoihuisha wazingatie umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika kazi zao.

Chanzo: habarileo.co.tz