Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima leo Jumatano, Machi 16, 2022, ametembelea eneo la ajali iliyotokea jana usiku wilayani Handeni na kuua watu wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Akiwa katika eneo la ajali, Malima amezungumza na baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo, ambao walidai gari iliyosababisha ajali haikuwa na taa.
Baadhi ya mashuhuda hao, walimueleza RC Malima kuwa ilitokea baada ya gari ndogo ya abiria iliyokuwa ikitokea Korogwe kuelekea Handeni, kugonga baadhi ya wananchi waliokuwa wakisaidia kuziba pancha kwenye gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa imeegeshwa pembeni ya barabara.
Shuhuda mmoja alida kuwa gari hiyo Toyota Hiace ilikuwa imepasuka tairi, hivyo wananchi walikuwa wanasaidia kubadili tairi.
"Kulikuwa na wanakijiji wanasaidia kubadilisha tairi, wakati Coaster inakuja, dereva akawa anaelekezwa asimame, lakini kwa sababu haikuwa na taa ikagonga wale wanakijiji waliokuwa wanasaidia na kuanguka bondeni, kwa hiyo waliopata ajali wengi ni wanakijiji," amedai shuhuda huyo.
Mkuu wa Mkoa aliongozana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo. Majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni wakiendelea na matibabu