Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gambo awaonya viongozi wanaohifadhi wahamiaji haramu

88627 Pic+gambo Gambo awaonya viongozi wanaohifadhi wahamiaji haramu

Mon, 16 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewatahadharisha baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wenye tabia ya kuwakaribisha wahamiaji haramu kuacha mara moja kwani kwa kufanya hivyo nao wanakuwa sehemu ya wahalifu.

Gambo aliyasema haya Leo Desemba 15, 2019 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali katika uzinduzi wa vikundi vya wafanyabiashara ya mifugo katika Soko la Kimataifa la Mifugo Eworendeke lililopo wilayani Longido mkoani Arusha. 

Amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kuwakaribisha wahamiaji haramu na kuishi nao kinyume cha sheria akiwataka kuacha kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria na taratibu za nchi yetu.

Gambo amesema kuwa, endapo watagundua mahali popote pale kuwepo kwa viongozi wa aina hiyo watakamatwa mara moja na kushtakiwa kwani nao ni sehemu ya  wahalifu .

Aliongeza kuwa, ukiwa kiongozi kazi yako kubwa ni kuhakikisha unakuwa mlinzi wa nchi yako katika kukemea uhalifu na uovu wowote ,na si kuwa chanzo cha uhalifu huo kama wengine wanavyofanya.

Akizungumzia kuhusu uwepo wa kiwanda hicho, Gambo aliwataka wananchi wa Longido kuhakikisha wananufaika ipasavyo na fursa ya uwepo wa kiwanda na mnada huo kwani wataweza kuondokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili ikiwemo soko la uhakika.

Aliwaagiza viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanufaika wa kwanza wa kiwanda na mnada huo wanakuwa wananchi wa Longido ili wanufaike rasilimali walizonazo na si watu wengine kutoka mbali.

"Changamoto hii nimewahi kukutana nayo sehemu nyingi sana unakuta kuna kiwanda kimejengwa kwa wananchi lakini wanaonufaika ni watu kutoka mbali badala ya wananchi wanaozunguka eneo hilo, ndio maana nimeweka mkazo hapa jamani viongozi wa wilaya naombeni sana msimamie hili kwa weledi na uaminifu mkubwa," alisema Gambo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Longido, Dk Steven Kiruswa amesema uwepo wa kiwanda hicho utawasaidia wananchi wake kujikwamua kiuchumi kutokana na kuwa na soko la uhakika huku akiwataka kutumia fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.

Kiruswa alimtaka mwekezaji huyo kuhakikisha anatangaza fursa zilizopo katika kiwanda hicho kwa wananchi wa Longido ili waweze kutambua mahitaji na fursa zilizopo katika kiwanda hicho .

Amesema ni vizuri kukawepo doria za mipakani ili kudhibiti utoroshaji  zaidi wa mifugo huku akiwataka wafugaji hao kutumia teknolojia mpya ya kuuza mifugo kwa mizani badala ya kukadiria kama ilivyokuwa hapo awali.

Naye Mwakilishi kutokana benki ya NMB, Oscar Rwechungura alisema kuwa, benki hiyo ipo tayari kushirikiana na wafugaji hao katika kuendeleza sekta ya mifugo nchini kwa kutoa elimu na mikopo mbalimbali kwa lengo la kujiendeleza.

Amesema wamekuwa wakitoa elimu kwa vikundi mbalimbali juu ya misingi bora ya biashara ili kuwawezesha kumudu ushindani katika biashara zao na kufahamu matumizi sahihi  ya fedha.

Chanzo: mwananchi.co.tz