Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gairo wajipanga kufufua zao la pamba

447668e09463b7cb08cd49c8f41dee6b Gairo wajipanga kufufua zao la pamba

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA kuhakikisha wanalifufua zao la pamba,viongozi wa wilaya ya Gairo mkoani Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Siriel Mchembe wameazimia kila mmoja kulima si chini ya ekari tatu za zao hilo ikiwa ni mfano kwa wananchi .

Hayo yaliazimiwa katika kikao cha siku mbili cha pamoja cha viongozi wa wilaya na wataalamu wa kilimo juu ya ufufuaji na uhimizaji wa zao la pamba kilichofanyika hivi karibuni.

Kikao hicho kilishirikisha wataalamu kutoka Bodi ya Pamba na wadau wa zao hilo.

Akizungumza katika kikao hicho Mchembe alisema wakati umefika kwa wakazi wa wilaya hiyo kulima mazao ya biashara na sio kutegemea mazao ya chakula ikizingatia kuwa ardhi ya eneo hilo inafaa kwa kilimo cha pamba.

Mchembe alisema kwa sasa kila kiongozi eneo lake msisitizo ni kilimo cha pamba na ofisa ugani yeyote katika wilaya hiyo atakayeshindwa kuhimiza wakulima wake kulima pamba itabidi aondolewe katika nafasi hiyo.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ameamua kutoa maagizo hayo kutokana na baadhi ya maafisa ugani katika vijiji na kata kutohimiza wananchi kulima zao hilo na kusema kuwa yeye kama kiongozi hatokubali mtaalamu wa kilimo alipwe mshahara bila kufanya kazi aliyoagizwa.

Aidha mkuu huyo wa wilaya ametoa siku saba kwa kila Ofisa Ugani aweke mpango kazi wa kilimo hicho ndani ya eneo lake na kisha kupeleka taarifa hiyo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili kujua ni wakulima wangapi watalima pamba msimu ujao wa kilimo.

Kwa upande wake Meneja wa huduma za usimamizi wa Bodi ya Pamba, Emmanuel Mwanguluma amesema lengo la serikali ni kuongeza uzalishaji wa pamba nchini kufikia tani milioni 1 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo Mwanguluma amesema kwa kufuata kikamilifu kanuni kumi za kilimo cha pamba wanategemea katika msimu huu wa pamba kupata ekari 500 ambazo zitatoa kilo laki 5 huku pia juhudi za uhamasishaji zikiendelea katika kanda hiyo ya mashariki ikiwemo mikoa ya Iringa,Morogoro,Pwani,Tanga na Kilimanjaro.

Naye mnunuzi mkuu wa pamba katika kanda hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Upami Agro Business Ltd Vitus Lipagila akiwataka maafisa hao ugani wakiwa maeneo ya kazi wafanye kazi iliyokusudiwa na watoe elimu ya mazao yote yanayolimwa katika maeneo yao kwani wanatakiwa waelewe wao ndio tegemeo la Taifa katika kilimo.

Chanzo: habarileo.co.tz