Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

GGM watenga milioni 76/- kukabili ajali barabarani

27069 Pic+ggm GGM watenga milioni 76/- kukabili ajali barabarani

Tue, 5 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

UONGOZI wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) umesema umetenga bajeti ya Sh milioni 76 kufanikisha mradi wa utoaji elimu ya usalama barabarani kwa makundi ya watumiaji wa barabara mkoani Geita.

Meneja Mwandamizi anayeshughulikia mahusiano ya taasisi za nje kutoka GGM, Manase Ndoroma alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi huo, utakaoanzia Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Alisema wamefikia uamuzi huo, baada ya kubaini ajali nyingi mkoani humo zinatokana na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani.

“Tunataka kudhibiti ajali, tukiacha ajali ziendelee jamii, haitakuwa salama na haitakuwa na ustawi, na sisi tunahitaji jamii iwe na ustawi ili biashara zetu zifanyike kwa amani kwa sababu usalama wa barabara na usalama wa raia ni sehemu ya mafanikio yetu”alisema.

Manase alisema ili kuifikishia jamiii elimu hiyo, GGM imepanga kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kufadhili mradi huo. Alisema kuwa bajeti waliyotenga, itatumika kuwalipa maofisa usalama barabarani watakaotoa elimu na kugharamia vyombo vya ufundishiaji na mahitaji mengine.

“Lakini pia zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi wetu wanaishi Geita mjini, watoto wao wanasoma hapa na familia zao zinatumia usafiri wa hapa, tunahitaji usalama walionao mgodini waupate pia nje ya mgodi, watu wetu wawe salama na jamii iwe salama,” alisema Manase.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani hapa, Swalehe Digega alisema elimu hiyo iliyofadhiliwa na GGM, itayalenga makundi yote ya watumiaji wa barabara yaani watembea kwa miguu, madereva wa bajaji, bodaboda, magari na waendesha baiskeli ambao ndiyo wengi zaidi mkoani hapa.

Digega alisema elimu itakayotolewa, itaongeza hamasa ya usimamiaji wa sheria na kanuni za usalama barabarani na kupunguza madhara yatokanayo na matukio ya ajali, ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu.

Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Wilaya ya Geita, Daniel Dotto aliwashukuru GGM na Jeshi la Polisi kwa kuanzisha mradi huo. Aliahidi kuwashirikisha viongozi wa vituo vya bodaboda, kuongeza hamasa na ushiriki wa madereva hao kupatiwa elimu hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz