Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Furaha ya Lucy nyuma ya Kisukari kwa miaka 18

55740 FURAHA+PIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pochi ya mwanamke haikosi vipodozi, manukato, simu na vitu vingine vidogo muhimu, lakini kwa Lucy John Bosco kitu muhimu zaidi kubeba katika pochi yake ni sindano za Insulin maalumu kwa ajili ya kudhibiti sukari mwilini.

Hayo yamekuwa maisha yake kwa miaka 18 sasa. Hata hivyo kisukari hakijaweza kuondoa tabasamu, kutafuta elimu na ari ya kujituma kufanya kazi mbalimbali ikiwamo kujitolea kutoa elimu hukusu kisukari na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza.

Akifahamu fika kuwa maisha yake yote yatagemea sindano za insulin, haachi kueleza namna ambavyo anayafurahia kwa kuwa amelitambua tatizo lake na kulikubali.

Alipata kisukari na miaka 14

Ilikuwa miaka 18 iliyopita akiwa shuleni nchini Uganda wakati huo akiwa na umri wa miaka 14 alipogundulika kuwa ana ugonjwa wa kisukari.

Alikuwa binti wa kawaida ambaye hakutegemea sindano kuishi, lakini maisha yake yalibadilika ghafla baada ya kula chakula kilichodaiwa kuwa na sumu.

Baada ya kutibu tatizo hilo ndipo likaibuka la kisukari ambalo kwa miaka 18 limemfanya aishi kwa kutegemea sindano na uangalizi wa hali ya juu wa mlo wake.

Alilazimika kurudi nchini na kuahirisha mwaka mmoja wa masomo akijiuguza.

“Bahati mbaya mwaka 2007 nikiwa nimerejea shuleni niliugua sana na kupoteza fahamu kwa muda mrefu na hali hiyo ilinikuta nikiwa ndani ya basi nikirejea nchini:

“Bahati nzuri nilipoingia kwenye basi nilimfuata kondakta na kumueleza hali yangu. Nilimwambia ninaumwa na nina kisukari na kama chochote kitatokea ahakikishe siwekewi drip la glucose. Ilikuwa bahati yangu kwa sababu nilipoteza fahamu na nilikuja kuamka wiki tatu baadaye nikiwa hospitalini mkoani Arusha,” anasimulia.

Tangu hapo tatizo linalomkabili ni la usahaulifu kwamba hata baada ya kuamka hakuwa akimtambua mama yake mzazi.

“Nina tatizo la kusahau lakini pia ninajua kukabiliana nalo, nikiona nasahau kitu najua tu sukari haipo sawa hivyo nafanya juu chini kuidhibiti kwa vyakula au sindano na insulin.”

Ni msomi wa usuluhishi, mawasiliano, lishe

Pamoja na changamoto za kisukari, Lucy ana shahada ya kwanza ya masuala ya usuluhishi wa migogoro na shahada ya uzamiri ya mawasiliano ya umma.

Pia, ana stashahada ya ushauri wa masuala ya kisukari na ulaji bora ambayo anasema alilazimika kusomea ili kuwasaidia wengine kutoathirika na ugonjwa huo.

“Nilipokuwa shuleni Kampala (Uganda) ndipo nilipata wazo la kusomea masuala ya usuluhishi kutokana na eneo la Kaskazini mwa nchi ya Uganda kuwa na migogoro inayohusisha vita, nilitamani sana kuona amani inakuwepo duniani kote ndio maana nikasomea fani hiyo.”

Kitu gani anakikosa

Lucy ambaye pia ni mtangazaji na mwandishi wa habari, anasema amejikubali na hakuna anachokikosa katika maisha yake kwani kila anachofanya anazingatia afya yake. “Nina kula kila kitu isipokuwa kwa kiasi, kwa mfano chipsi mayai mara moja moja nakula kidogo sana kwa hamu tu, lakini zaidi nazingatia chakula bora,” anasema.

Changamoto pekee anayokutana nayo ni jamii kutoipokea elimu anayotaka kuwapa wakitaka kuwezeshwa kuhudhuria semina zake.

“Inaniumiza sana pale ninapotaka kumpa mtu elimu naye anauliza nikija nitalipwa. Hii ninaweza kusema ndio changamoto pekee ninayokutana nayo katika safari yangu ya kisukari katika upande wa kutoa elimu,” anaeleza.

Awekeza kuelimisha watoto

Pamoja na kuelimisha makundi mbalimbali kuhusu ugonjwa wa kisukari, Lucy anasema mwaka huu amepanga kuelekeza nguvu kuwaelimisha watoto.

“Ulaji mbovu unaanzia utotoni, mara nyingi utasikia mtoto hapendi mboga za majani au chakula fulani. Inabidi tuwafundishe watoto faida na hasara za vyakula ili wanapochagua wajue umuhimu wake,” anafafanua.

Kwa nini elimu ya kisukari?

“Kwa mfano mimi natumia siyo chini ya Sh150,000 kwa wiki kwa ajili ya matibabu yangu, wengine wanatumia dozi kubwa zaidi yangu ina maana wanatumia fedha nyingi zaidi,” anasema.

“Kama fedha hizi mtu angeziweka katika biashara au shughuli nyingine ya maendeleo kwa mwaka mzima angekuwa amepiga hatua gani?”

Anasema mbali na kutumia fedha nyingi kujitibu, wapo wanaopata ulemavu kutokana na kisukari ikiwamo kukatwa viungo vya mwili au kupata upofu.

“Nguvu kazi ya Taifa inapotea, wengi wanapata ulemavu kwa maana hiyo kama siyo kisukari huenda watu hawa wangeisaidia jamii au Taifa kufikia hatua fulani,” anasema.

Pia, anasema Serikali isingetumia fedha nyingi kutibu wagonjwa wengi kama wangeelimishwa kwa sababu wapo wanaopata matatizo kwa kutokujua namna ya kujikinga.



Chanzo: mwananchi.co.tz