Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fukwe Dar zatekeleza agizo la JPM

Ffb964cf869cf39018c7cc5594604a01 Fukwe Dar zatekeleza agizo la JPM

Tue, 2 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAMILIKI wa fukwe mkoani Dar es Salaam, wameanza kutekeleza agizo la Rais John Magufuli linalotaka wananchi wasizuiwe kufika baharini katika maeneo hayo kutembea, kuogelea, kupumzika na hata kufanya mazoezi.

Awali, Ufukwe wa Coco uliopo Oysterbay wilayani Kinondoni ndio pekee ambapo mwananchi wa kawaida walikuwa wanaweza kuingia bila usumbufu.

Kwa muda mrefu ilikuwa vigumu kwa wananchi wa Kigamboni kufurahia rasilimali hiyo kutokana na wamiliki kutoacha nafasi za kuruhusu watu kupita kwenda ufukweni.

Katika Wilaya ya Kigamboni, Ufukwe wa Ulongoni unaomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ulikuwa pekee ambao wananchi wanaingia bure na kufurahia huduma zikiwemo za baa, kubembea na nyinginezo.

Wananchi wanaoingia kupitia ufukwe huo wamekuwa na nafasi ya kuendelea kutembelea fukwe nyingine za karibu zikiwemo za Mikadi ya Wazungu na Mikadi ya Kawaida.

Kutoka fukwe moja kwenda nyingine hakukuwa na njia hivyo wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kupata njia ya kuingilia kwenda ufukweni kwa kuwa walitakiwa kulipa viingilio kwenye ufukwe wanapoingilia.

Viingilio hivyo vilikuwa kati ya Sh 2,000 na Sh 10,000 kwa mtu mmoja. Fukwe zilizopo karibu na feri kiingilio ni Sh 2,000 kila siku kuanzia Jumatatu hadi Jumapili na mteja anaruhusiwa kuingia na vyakula na vinywaji vyake.

Kuanzia Mji Mwema kuelekea Sunrise, Kipepeo, na South Beach, viingilio ni Sh 10,000 kwa kila siku za mwishoni mwa wiki huku mteja akiwa haruhusiwi kuingia na vinywaji wala vyakula.

Katikati fukwe hizo katikati ya wiki, hakuna viingilio, lakini wananchi hawaruhusiwi kuingia na vyakula wala maji.

Ili kutekeleza agizo la Rais Magufuli kutaka wananchi wasizuiwe kufika ufukweni, wamiliki wa fukwe wamelazimishwa kuacha njia zinazowawezesha wananchi kupita kwenda ufukweni bila ya kuingia kwenye sehemu ya mmiliki aliyotenga kwa ajili ya wateja wake wanaolipia.

Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kigamboni, Juevenalise Mauna alilieleza HabariLEO kuwa, ofisi yake ndiyo yenye jukumu la kusimamia fukwe zote za wilaya hiyo, na imeanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli kwa kulazimisha wamiliki wa fukwe kuacha nafasi kwa wananchi kupita kwenda baharini.

Alisema awali wakati wa upangwaji wa mipango miji, hawakuacha nafasi za wananchi kupita kwenda fukweni kwa kuwa waliuza viwanja vya fukweni kwa kuunganisha plot, lakini kwa sasa wamelazimisha ziachwe njia.

“Kwa fukwe zaidi ya 20 kuanzia Feri hadi Kimbiji kuna njia za wananchi kupita kwenda baharini kwa kuwa ni haki yao kwenda kucheza, kuogelea na kufanya shughuli nyingine mbalimbali fukweni,” alisema Mauna.

Alisema wawekezaji waliokataa kutoa ushirikiano wamechukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa fukwe kama ilivyofanyika kwa Ufukwe wa Kwa Frola uliopo Somangila aliosema umerejeshwa serikalini.

Mkazi wa Geza Juu, Juma Hamza, alilieza gazeti hili kuwa, sasa wanaweza kufika fukweni na kufurahia maisha.

Hamza alisema awali alikuwa akilazimika kwenda hadi ufukwe wa Jeshi Ulongoni ili aingie ufukweni kuogelea na kisha kurudi tena nyumbani kwake Geza Juu na alikuwa akitumia nauli ya Sh 800.

HabariLEO lilipotembelea Wilaya ya Kinondoni zilizopo fukwe za Mahaba, Dynast, Hawaii, Africa Raggae, Free Gate, Coco Land na Saigoni, lilishuhudia wananchi wakipita na kuingia bure kucheza kwenye maji na kuogelea.

Mmiliki wa Ufukwe wa Dynast, Manase Mwakale, alisema licha ya uwekezaji wa vifaa vya kisasa likiwemo jukwaa la muziki, majiko, baa na ukumbi wa muziki wananchi wanaruhusiwa kupita kwenda ufukweni.

Alisema mwananchi anaweza kununua kinywaji akiwa ndani ya eneo hilo la Dynast na hata kama hana fedha ya kinywaji, anaruhusiwa kukaa kwenye viti na kupumzika au kwenda kuogelea.

Alisema: “Hii ilikuwa ni sehemu ya wavuvi ambapo niliingia nao makubaliano kuwa niwekeze na wao waje kuniuzia samaki na pia yapo makubaliano yenye tija kwetu sote, hivyo hata wananchi mimi sina haja ya kuwazuia kuingia muda wote saa yoyote.”

Kamishina wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Idrisa Kayera alisema, nchini maeneo ya fukwe yote ni ya umma hivyo si sahihi kuwatoza fedha wananchi.

Alisema Sheria ya Mipango Miji ya Mwaka 2007 imebainisha maeneo hayo kuwa ya umma na yanalindwa na sheria hiyo.

“Ndio maana hata hoteli zilizojengwa kwenye fukwe hizi nyingi ikiwemo Sine Club zina uzio kutengenesha eneo lao na eneo la fukwe ambalo ni la umma.

Kayera alisema, pia sheria ya mazingira chini ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inasema kuanzia mita 60 kutoka baharini ni eneo la fukwe na maji na halipaswi kuingiliwa na mtu.

Chanzo: habarileo.co.tz