Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Foleni zapungua Dar zahamia Moshi

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi/Mwanza. Ile adha ya foleni za magari iliyokuwa katika Jiji la Dar es Salaam imehamia Moshi.

Msongamano mkubwa wa magari uliojitokeza kwa saa sita mfululizo juzi hadi saa tatu usiku ni hali ambayo haijazoeleka kwa watumiaji wengi wa barabara mjini Moshi ambao walilazimika kutumia muda mrefu kutoka eneo moja kwenda lingine.

Dalili za msongamano zilianza kujitokeza tangu juzi asubuhi na ilipofika saa 10 alasiri, hali hiyo ilijidhihirisha hasa katika ni barabara kuu ya Njiapanda ya Himo hadi Mailisita na barabara za katikati ya mji kwenye masoko na maduka makubwa huku magari yakikosa maeneo ya maegesho katikati ya mji.

Mkurugenzi wa Moshi Hugos Garden, Bosco Simba alisema msongamano wa magari haukuwa jambo la kawaida na ilimchukua muda mrefu kufika nyumbani.

“Huwa natoka hapa Hugos hadi nyumbani pale Mjohoroni sanasana natumia dakika 10 lakini jana (juzi) usiku nilitoka hapo mzunguko wa YMCA hadi nyumbani nikatumia dakika 60,” alisema.

Dereva wa magari ya kusafirisha watalii, Haji Sadiki alisema msongamano ulioshuhudiwa juzi usiku ulikuwa si wa kawaida.

Wakati Moshi wakilia na wingi wa magari, Mwanza hali ni tofauti. Jiji hilo limeelezwa kuwa na idadi kubwa ya watu.

“Unajua kwenye sikukuu kila mmoja anataka ale na kuvaa vizuri zaidi ya siku nyingine na huduma hizi nyingi zipo mjini hivyo hilo linachangia kuongezeka kwa watu wakati wa kipindi hiki,” alisema Faustine Grervaz mkazi wa Nyegezi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema jana kwamba ameshuhudia wingi huo wa watu tofauti na alivyozoea.

“Hata mimi nimezunguka maeneo mbalimbali jana (juzi) leo (jana), nimeshuhudia kuwapo kwa watu wengi. Mwaka jana sikuwapo lakini hata askari wangu wameniambia kuwa watu ni wengi kuliko wa mwaka jana,” alisema Shanna.



Chanzo: mwananchi.co.tz