Fisi wanne wanaosadikiwa kushambulia na kuua watu katika Kata ya Kasenyi, wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza wameuawa na wawindaji wa jadi kutoka wilayani Misungwi.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kasenyi, Juma Bupamba amethibisha kuuawa fisi hao.
Amesema wameuawa leo Machi 25, 2024 saa 11.00 jioni.
Ameeleza wawindaji hao wametumia takribani dakika 90 kuwaua wanyama hao.
Ofisa mtendaji huyo amesema baada ya kuona matukio ya watu kushambuliwa na fisi yamekithiri; na wananchi walichanga fedha kuwaita wawinda hao kutoka Kata ya Mbalika wilayani Misungwi.
Mkazi wa Kijiji cha Kasenyi, Amon Jonathan amesema fisi hao walikuwa tishio kwao, hivyo wanaamini watapa ahuweni.
Matukio ya fisi kushambulia na kuua watu yameripotiwa kwenye kata za Kasenyi, Chifunfu, Katunguru na Buyagu.
Watu watatu wamefariki dunia kwa kushambuliwa na fisi katika matukio tofauti wilayani Sengerema kati ya Januari hadi Febaruari 24, mwaka huu.
Tukio la kwanza lilitokea Januari 15, 2024, saa 12.30 jioni, kwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyakahako, Kata ya Chifunfu wilayani Sengerema, Sadiki Mashaka (16) kushambuliwa na fisi alipokuwa akichanja kuni mlimani.
Mwingine ni Mkazi wa Kijiji cha Lukumbi, Kata ya Chifunfu wilayani humo, Mkabagobi Sibanga (70), aliyefariki dunia Januari 29, 2024, saa 11.30 alfajiri, baada ya kushambuliwa na fisi akielekea shambani kuvuna mahindi.
Katika tukio lingine, mtoto wa miaka sita, Adela Shimba, mkazi wa Kijiji cha Kafundokile, Kata ya Kasenyi wilayani humo aliuawa na fisi Februari 16, 2024 alipokuwa ameambatana na bibi yake kwenda kuchota maji mtoni.
Taarifa za matukio hayo zimethibitishwa na Mkuu wa Idara ya Wanyamapori katika Halmashauri ya Sengerema, Paul Ponsian alipozungumza na Mwananchi Digital hivi karibuni.
"Kumekuwa na ongezeko la matukio ya fisi kushambulia wananchi, ndiyo maana tumeanza kuwasaka na kuwauwa. Tunawaomba wananchi waendelee kutusaidia kutoa taarifa na ushirikiano ili tuwatokomeze wanyama hao wanaovamia wananchi,” amesema Ponsian.
Amesema kupitia misako iliyoendeshwa na maofisa wa Mamlaka ya Wanyamapori (Tawa) wilayani Sengerema, fisi watano wameuawa.
Amesema misako hiyo itakuwa endelevu ili kuhakikisha wanyama hao hawahatarishi maisha ya wananchi.