Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fisi aua kondoo wanne, nguruwe wawili Mufindi

Fisi Aua Nguruew.jpeg Fisi aua kondoo wanne, nguruwe wawili Mufindi

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Sintofahamu imezuka kwa wananchi wa Kata ya Makungu Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, baada ya kondoo wanne, nguruwe wawili kuuawa, pamoja na kuku mmoja akijeruhiwa, huku tahadhari ikitolewa kwa wananchi hao.

Hata hivyo, Afisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Ndimyake Mwakapiso amesema wanyama hao wa kufugwa hawajajeruhiwa na Simba kama ilivyodaiwa hapo awali, isipokuwa ni mnyama aina ya fisi.

Akitolea ufafanuzi wa sintofahamu hiyo leo Alhamisi July 6, 2023 Mwakapiso, amesema kuwa taharuki hiyo imetokea kwa wananchi wa Kijiji cha Mabaoni na Lole wakihofu kuwa huenda simba ndiyo wamehusika katika tukio.

Kufuatia uchunguzi uliyofanywa na ofisa wanyamapori, umebaini kuwa ni fisi ndiye aliyeua na kujeruhi mifugo hiyo.

"Fisi huyo amejeruhi mifugo ya mwananchi mmoja ambaye amefahamika kwa jina moja la Chavagale ambapo kondoo wake wanne wamekufa baada ya kupata majeraha ambayo yametokana na kucha za mnyama huyo," amesema ofisa huyo.

Aidha Mwakapiso amewataka wananchi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari huku jitihada za kumsaka fisi huyo zikiendelea ili asiweze kuendelea kuleta madhara mengine zaidi.

"Niwaombe wananchi kushirikiana kwa pamoja kuweza kumsaka fisi huyo ili asije kuleta madhara kwa binadamu, tuhakikishe mara tu anapoonekana, basi tujue kuwa anatakiwa kuuawa," amesema Mwakapiso.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Kijiji cha Mabaoni, Thobias Jonas Mkwama amethibitisha kupata taarifa hizo toka kwa mmiliki wa mifugo huku akisema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa.

"Baada ya kupokea taarifa hiyo tuligonga kengele kwa ajili ya kuwakusanya wananchi na kuwaeleza juu ya kuuawa kwa mifugo hiyo, hata hivyo alishindwa kuthibitisha iwapo ni simba walio husika na kadha hiyo,” amesema na kuongeza;

“Unajua, kama wiki tatu zilizopita, tulisikia kwenye vyombo vya habari kwamba kuna sehemu simba wamevamia na kula mifugo nasi tulihisi hivyo baada ya kuthibitisha kweli mifugo hiyo imeuawa.”

Kwa upande wake, Ofisa Mifugo Kata ya Makungu Evaldo Mavika amesema baada ya kufika eneo la tukio na kufuatilia alama za nyanyo za mnyama huyo, walifanikiwa pata kilo 3 za nyama pekee ambazo zilikuwa zimesalia katika eneo hilo.

Hata hivyo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meingataki amesema Simba waliokadiriwa kuwa watano, waligawanyika katika makundi mawili, moja limerudi hifadhini na lingine lipo katika Kijiji cha Isingo karibu na mashamba ya mwekezaji (hakutajwa jina) ambako kuna msitu mnene.

Chanzo: Mwananchi