Wakuu wa shule za sekondari Manispaa ya Shinyanga wameeleza fedha za kupambana na ugonjwa wa Covid-19 zinamaliza changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika manispaa hiyo.
Walisema hayo juzi mbele ya Mbunge wa Shinyanga Mjini, Probas Katambi kutokana na fedha za Covid-19 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kolandoto, Deus Maganga na Mkuu wa Shule ya Sekondari Uzogole, Cosmas Nkoko walisema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati wakitoa taarifa kwa Mbunge huyo kuhusu ujenzi wa vyumba vya madarasa alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo.
“Ujenzi wa vyumba vya madarasa utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani, hivyo hatuna budi kumpongeza Rais wetu kwa jitihada alizozifanya kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira mazuri,” alisema Nkoko.
Katambi ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira alifanya ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari na shikizi katika Manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wataalamu, pamoja na kamati ya siasa ya CCM wilaya.
Pia alipokea taarifa kutoka kwa wakuu wa shule kuwa madarasa yamekamilika na changamoto ya upungufu wa vyumba hivyo kwa baadhi ya shule umepungua.
“Wananchi wa Jimbo la Shinyanga tumpongeze Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa ambapo watoto wetu wanaoingia kidato cha kwanza mwakani watasoma katika mazingira mazuri sababu vyumba vya madarasa vipo vya kutosha,” alisema Katambi na kuongeza:
“Nimekagua pia ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa katika Shule ya Kolandoto, kwa kweli nimeona thamani yake ya fedha, mmejenga kwa ubora unaotakiwa ambapo licha ya kujenga vyumba viwili vya madarasa kwa Sh milioni 40, lakini mmejiongeza na kujenga ofisi moja ya walimu.”
Katambi aliwapongeza wananchi wa Shinyanga kwa kumuunga mkono Rais Samia kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa na kutoa nguvu kazi ikiwamo kushiriki kwenye uchimbaji msingi.