Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia zakutana kujadili mahari ya marehemu

90241 Mahari+pic Familia zakutana kujadili mahari ya marehemu

Mon, 30 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Mazishi ya mwimbaji wa kwaya wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) jijini Arusha, Mary Richard (29) aliyeuawa kwa kukatwa na shoka kichwani na mumewe, yameshindikana kutokana na ndugu zake kusubiri mahari ambayo haikulipwa.

Mumewe, Moses Pallangyo (28), ambaye pia ni mwanakwaya, hajaonekana tangu taarifa za mauaji hayo zilipoibuka.

Lakini ndugu za wawili hao wameingia katika majadiliano ya mahari, huku ndugu wa mwanamke wakitaka ilipwe ndipo wamzike.

Jeremiah Peter, ndugu wa marehemu Mary, alisema tayari vikao vya familia mbili vimeanza ili kujadili mahari na baadaye taratibu za mazishi.

“Moses hakuwahi kulipa mahari ya kuishi na ndugu yetu. Sasa, kwa utaratibu, licha ya kilichotokea lazima mahari ilipwe kwa ndugu ili marehemu azikwe,” alisema.

Dada mkubwa wa Moses, Jenipher Pallangyo pia aliiambia Mwananchi jana kuwa walikuwa na kikao cha suala hilo kabla ya kutangaza siku za mazishi.

Hata hivyo, alisema hadi jana mchana, kiwango kamili ambacho kinahitajika kulipwa kilikuwa bado hakijajulikana, lakini anaamini muafaka utapatikana.

“Ni kweli kuwa Moses alikuwa hajalipa mahari. Sasa kwa taratibu zetu huwezi kumzika binti kabla hajalipiwa mahari na wazee nyumbani leo (jana) wapo na familia ya Mary ili kujua mahari kisha ilipwe ndipo mwili uzikwe,” alisema.

“Pia bado tunafuatilia kujua kanisa la FPCT ambalo alikuwa anasali Moses na marehemu mkewe ili kupata taarifa zao,” alisema.

Moses Pallangyo, maarufu kama Moses Libaba, anatuhumiwa kumuua Mary kwa kumkata shoka kisha kukimbia.

Pallangyo alikuwa amekwenda kwa wazazi wake walio kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru wiki tatu zilizopita na mkewe huyo kumtambulisha.

Alisema Moses ni mtoto wa tano, kati ya watoto saba katika familia yao na kwa muda mrefu alikuwa jijini Arusha akijihusisha na kuimba kwaya na alifanikiwa kurekodi nyimbo kadhaa.

Hadi jana mchana kikao cha mahari na mazishi kilikuwa kinaendelea nyumbani kwa wazazi wa Mary katika eneo la Njeku kata ya Embaseni.

Marehemu ameacha mtoto mmoja ambaye alizaa kabla ya kuolewa na Moses.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi mkoa, Jonathan Shana, alisema jana kuwa bado polisi inamsaka Moses Pallangyo kutokana na mauaji hayo.

Kamanda Shana alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa kuhusu sehemu alipo Moses, kujitokeza kutoa taarifa ili kufanikisha upelelezi wa tukio hilo na kujua chanzo cha mauwaji hayo ambayo hadi sasa chanzo chake hakijulikani huku wanaomfahamu Mary na Moses wakisema kwamba wawili hao hawakuwa na ugomvi wowote kabla ya mauaji hayo kutokea.

Chanzo: mwananchi.co.tz