Watu kadhaa wamenusurika kifo katika Mtaa wa Mrara Wilayani Babati Mkoa wa Manyara kufuatia nyumba ya Serikali ambayo wanaishi Watumishi wa Halmashauri (Mke na Mume) kuwaka moto na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa ndani.
Shuhuda aitwaye Osante Osea amesema kuwa "Mimi naishi jirani hapa wakati moto unaanza nilipewa taarifa na Mtoto wa hapa kwamba kwenye chumba cha Mzee kuna moto unawaka nikaenda kujaribu kutoa vitu lakini moto ukaanza kuwa mkubwa na moshi kutanda nikaanza kuwatafuta Zimamoto wakati huo kuna mtoto Mlemavu alikuwa ndani anashindwa kujua cha kufanya ndipo nikamshika na kumtoa nje"
“Baada ya kuwapigia Zimamoto walikuja kwa wakati lakini walishindwa kuuthibiti moto huo baada ya gari kuisha maji hali iliyowalazimu kuondoka tena kufuata maji wakati huo nyumba ikiendelea kuteketea kwa moto”
Kwa upande wake Inspekta Misieki Likindaasaro kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Manyara amesema baada ya wao kufika walikuta moto umefika hatua ya nne ambapo hatua hiyo moto unakuwa umeshika kila kitu huku kulingana na aina ya material yaliyotumika katika ujenzi wa nyumba hiyo ilikuwa ni vigumu kuuthibiti moto huo.
"Tulihitaji maji mengi sana kuuzima huu moto kulingana na aina ya material (mbao) lakini kwa bahati mbaya Mkoa wetu una gari moja tu la kuzima moto na umbali wa kujazia maji ni KM 10 na lina uwezo wa kubeba Lita 4000 za maji na Lita 500 za kemikali maalumu za kuzimia moto kwahiyo kwa presha iliyokuwa inatumika ilikuwa inachukua dakika 10 maji kuisha kwahiyo inatubidi kufuata maji tena ila kungekuwa na gari mbili pengine tungeweza kuudhibiti huu moto ila hakuna chochote ambacho tumeweza kukiokoa ila zaidi tumethibiti moto usiende kwa majirani huku chanzo cha awali cha moto huu kikiwa bado hakijafahamika"