Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yamsaka kijana wao anayedaiwa kuzama baharini

Baharinipic Familia yamsaka kijana wao anayedaiwa kuzama baharini

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Familia ya Awadhi Matondo (17) anayesadikika kuzama na kufa maji imelazimika kuweka kambi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi kwa siku mbili sasa kuutafuta mwili wake.

Familia hiyo ya watu zaidi ya 10 ikiongozwa na baba mzazi, Hassan Matondo wamekuwapo ufukweni hapo eneo la Mji Mwema huko Kigamboni tangu Jumamosi wakiutafuta mwili huo ambao ni kati ya miwili iliyopotea kabla mmoja kupatikana Jumamosi.

Kwa mujibu wa baba mzazi wa marehemu, Awadhi alikwenda ufukweni hapo Jumamosi asubuhi kucheza mpira akiwa na wenzake watano. “Walipomaliza kucheza mpira waliamua kuogelea, hakuwa mgeni wa maji lakini nahisi siku ilikuwa imefika,” alisema mzee huyo kwa huzuni.

Tukio hilo, alisema limetokea ikiwa imepita siku moja tangu amuonye juu ya michezo ya majini kufuatia kifo cha kijana wa jirani yao ambaye alifariki akiogelea.

“Ijumaa tu nilikuwa nikimuonya kuhusu michezo ya maji, Jumamosi yametokea haya, ni mipango ya Mungu,” alisema Matondo.

Awadhi alikuwa akisubiri matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, kwani alikuwa mwanafunzi wa Sekondari ya Mizimbini iliyopo Kibada, hukohuko Kigamboni.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Justine Kimambo alisema vijana hao baada ya kumaliza kucheza mpira waliingia kuogelea, kitu ambacho ni kawaida.

“Lakini inaonekana maji yalikuwa na nguvu na yalianza kuwashinda, walipiga kelele watu waliokuwa karibu walifanikiwa kuwaokoa watatu kati ya watano na wawili hawakuonekana,” alisema.

Katika jitihada za kuendelea kuwatafuta, alisema mwili mmoja ulipatikana ufukweni na mmoja ndiye anaendelea kutafutwa mpaka sasa.

“Unajua vijana wanapoingia kwenye maji wakiwa wengi huwa wana kawaida ya kupiga kelele kwa mambo yao, sasa hizi zilikuwa za kuhitaji msaada lakini hadi watu waje kugundua muda ulikuwa umepita,” alifafanua Kimambo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mjimwema, Darusi Mohammed alisema taarifa za kuzama kwa vijana hao alizipata mtaani na hazikuwa rasmi.

“Kwa hiyo hata sasa nilikuwa najua wote wameshapatikana kwa sababu hawakuja ofisini kuripoti,” alisema huku akibainisha kuwa jitihada bado zinaendelea kuupata mwili huo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Richard Ngole alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku jitihada za kuupata mwili wa kijana huyo zikiendelea.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live