Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yamlilia Mtanzania aliyeuawa Israel

Mtanzaniaaaa Israel.jpeg Familia yamlilia Mtanzania aliyeuawa Israel

Sun, 19 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rombo. Familia ya Mtanzania aliyefariki nchini Israel, Clemence Mtenga, imesimulia namna ilivyokuwa ikiwasiliana na kijana wao akiwa nchini humo hadi Oktoba 7, 2023 kundi la Hamas lilipovamia Israel na kuteka watu akiwemo kijana huyo.

Simulizi ya familia hiyo inakuja wakati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ikiwa imetoa taarifa ya kupokea taarifa za kifo cha Clemence aliyekuwa miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine waliokuwa hawajulikani walipo baada ya vita kati ya Israel na Hamas kuanza.

Taarifa hiyo iliyotolewa na wizara hiyo imesema marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Tanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

Akizungumza leo Novemba 18 katika Kijiji cha Kirwa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, baba mzazi wa marehemu ambapo amesema mwanawe alihitimu Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro Agosti, 2023 na ndipo alipochaguliwa kwenda nchini Israel kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Mtenga amesema Clemence ambaye alikuwa mtoto wake wa nne wa kuzaliwa alikuwa mtu mwenye bidii na mwenye kujituma na kwamba licha ya tukio hilo kuwaumiza kama familia na kuwaachia pengo kubwa, anaamini ni ajali kama ajali nyingine.

"Mwanangu alikuwa na bidii sana kwenye masomo na alikuwa akifuatilia sana elimu na katika eneo hili alikuwa hafanyi mchezo wala hakuwa mzembe na hata alikuwa akija nyumbani mambo yake yalikuwa yamenyooka na akifanya mambo yake hayakuwa na dosari.

"Alipohitimu masomo yake ya chuo kikuu, aliniambia kuwa amepata bahati ya kuchaguliwa kwenda Israeli, nami nikamwambia kama umebahatika ni sawa. “Akaja nyumbani akakaa kama wiki mbili ndipo akaniambia ameitwa Morogoro kwa ajili ya kuungana na wenzao ili kwenda Dar es salaam kwa ajili ya kuanza safari kwa pamoja,” anasimulia Mtenga.

Baba mzazi wa Clemence Mtenga, Felix Mtenga (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kifo cha mwanaye kilichotokea nchini Israeli, kushoto ni Boniphace Mtenga mwenyekiti wa ukoo wao. Picha na Florah Temba. Ameendelea kusimulia kuwa, baada ya mwanawe kuondoka na kufika nchini Israel walikuwa na tabia ya kuwasiliana kila Jumapili kujuliana hali, hadi ilipofika Oktoba 7, aliposikia machafuko ambapo alimpigia akawa hapatikani.

"Niliposikia kuna mashambulizi Israel nikampigia nikawa simpati, niliendelea kumtafuta hata Oktoba 8 mpaka10 lakini nikawa simpati, nikawajulisha dada zake na kuwauliza kama wao wamewasiliana lakini nao walisema hapatikani, wakaniambia ni hali ya mawasiliano," amesema.

Ameeleza kuwa waliendelea kumtafuta bila mafanikio mpaka siku walipopata taarifa kuwa yeye na mwenzake walitekwa na hawapatikani.

Anasema baada ya kupata taarifa hizo, walianza kuwasiliana na balozi wa Tanzania nchini Israel lakini Clemence hakupatikana.

"Jitihada ziliendelea kufanywa na Serikali, watu wa haki za binadamu na wengine na baadae tuliambiwa vinahitajika vipimo vya vinasaba (DNA) na wiki mbili zilizopita vilichukuliwa vipimo vya vinasaba na tukawa tunasubiria majibu.

“Juzi nilizungumza na balozi ndipo akaniambia baada ya vinasaba kufika kule katika utambuzi ndipo wakagundua kwamba Clemence ni marehemu na jana mkuu wa wilaya alikuja kuniletea taarifa kuwa hatuko nae tena," anasema.

Aidha baba huyo amesema hana cha kusema kuhusiana na tukio hilo na anaamini kilichompata mwanawe ni ajali kama ajali nyingine na kuomba Serikali isikatishwe tamaa na tukio hilo katika kusaidia vijana kwenda kujifunza Israel

"Hapa sina cha kusema na kilichompata mwanangu mimi naona ni bahati mbaya, na ni ajali kwa sababu Israel wamekuwa wakienda vijana kujifunza na wanarudi na serikali imekuwa ikiwapeleka na wanarudi salama bila shida."

Kwa uoande wake Boniphace Mtenga ambaye ni mwenyekiti wa ukoo na msemaji wa famila hiyo, amesema wamepokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa na kwamba kwa sasa wanasubiria taratibu za serikali za kuurudisha mwili nchini ili taratibu za mazishi ziendelee.

"Familia tumepokea kwa masikitiko makubwa sana, maana kijana huyu tulikuwa tunamtegemea tukijua atakapohitimu masomo yake, atakuja kuinua wadogo zake na ndugu zake wengine, hata ukoo tulimtegenea lakini yale matazamio yetu na baba yake yamekatwa ghafla," amesema.

Amesema mpaka sasa hawajui alifikwa na umauti kwa namna gani kama alipigwa risasi au nini kilitokea na kwamba wanasubiri mwiki ufike ndipo wajue nini ambacho kilitokea.

Aidha amesema wamefanya nawasiliano na Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambapo wametakiwa kusubiri taratibu za Serikali kurudisha nwili nchini.

"Kwa sasa bado hatujapanga taratibu za maziko, katibu mkuu alituambia wataendelea na mawasikiano na balozi nchini Israel na majibu yatapatikana kuanzia Jumatatu," amesema.

Akizungumzia mashambulizi hayo yanayoendelea nchini Israel, alisema ipo haja ya kusitishwa kwa kuwa wanauawa watoto, vijana na watu wengine wengi wasio na hatia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live