Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yakimbia makazi kwa mauzauza

53373 Pic+familia

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Ni ushirikina? Hilo ndilo swali wanalojiuliza wakazi wa Uru Mwasi - Kaskazini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kutokana na familia moja kuteswa na mauzauza kiasi cha majirani kuanza kuogopa kuipa hifadhi.

Mauzauza hayo yanaiandama familia ya Justine Mushi na yameifanya kukimbia makazi yao kutokana na mawe kudaiwa kudondoka kutoka juu na moto kuwaka bila kufahamu unakotokea.

Ukisikiliza simulizi ya familia hiyo ya watu saba, unaweza kuhisi kuwa ni hadithi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiteseka, kufuatwa kila waendako na kusababisha kuogopwa hata na wananchi wenzao. Moja ya vimbwanga ambavyo vimeifanya familia hiyo kuhama nyumba ni pamoja na mawe kudondoka ndani ya nyumba usiku na moto kuwaka.

Hali hiyo imeitesa familia hiyo kwa kipindi cha miezi miwili na imelazimika kukimbia makazi ambapo wakiwa kwa majirani, mama mzazi wa Justine, Ermina Mushi alikimbilia Dar es Saalam kwa mtoto wake baada ya mauzauza hayo kumfuata hadi kwa majirani.

Hivi karibuni nyumba ya Romani Njau, baba mdogo wa Justine ambaye alilazimika kukimbia makazi yake, iliteketea moto baada ya mawe kudondoka ndani na moto kuwaka.

Moto huo uliowaka kwa nusu saa bila kuokoa chochote, ulianzia katika chumba ambacho alikuwa akilala Justine na kuibua hofu kubwa kwa majirani wengine ambao walikuwa wakiihifadhi familia hiyo.

Kufuatia hali hiyo, majirani wanaogopa kuendelea kuwahifadhi na kuiomba Serikali kuwasaidia.

Reuben Temba, mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho anaiomba Serikali kumchukua Justine na kumtafutia hifadhi kutokana na kuogopwa na wanakijiji kwa matukio yanayomtokea.

Anasema kwa hali ilivyo sasa hakuna mwananchi anayethubutu kumsogelea.

“Kwa kweli hakuna mtu anayeweza kumsaidia kijana huyu aliyeachwa hapa kijijini bila familia yake kutokana na majanga yanayowatokea kila waendapo,” anasema Temba.

“Ukiwa naye karibu vitu vya ajabu vinatokea kama mawe kurushwa, moto kuwaka au yeye kupigwa na watu wasioonekana.”

Mke aeleza chanzo cha tatizo

Digna Mushi, mke wa Justine anasema kuanzia Aprili 2018, mtoto wake wa kwanza Elizabeth Justine alikuwa akipigwa usiku na watu wasioonekana ndipo walipoanza kuzunguka huku na kule kwenye maombi makanisani.

Anasema pia mtoto huyo alikuwa akifika shuleni anaanguka na kuzimia, na wakati mwingine kuanza kutokwa na damu puani na anapopelekwa hospitali anaonekana hana tatizo lolote la kiafya.

“Baada ya kuhangaika sana mume wangu aliamua kwenda kwa mganga na mtoto ambapo alipewa dawa na nyingine alipewa mama mkwe wangu ambayo alikuwa akiifunga kiunoni,” anasema Digna.

Anasema ilipofika Desemba mauzauza hayo yalizidi na ilimlazimu kuondoka na kwenda kwa wazazi wake kwa sababu alikuwa na mtoto mchanga.

“Nilikaa nyumbani kwa muda wa wiki mbili, baadaye mume wangu akanifuata na kuniambia kuwa tatizo la mawe kudondoka ndani ya nyumba yetu limeisha nikaamua kurudi.”

Anasema baada ya kurudi na kukaa siku tatu, tatizo hilo lilirudi tena kwa ukubwa ambapo mkwewe alikuwa akilia usiku akipigwa na vitu visivyoonekana.

Anasema, “baadaye mawe yakaanza kudondoka yakimwandama mume wake na mama mkwe.”

“Nilikuwa naona mawe yanadondoka, lakini mtu anayerusha haonekani. Niliamua kuondoka hadi leo sijarudi.”

Anasema, baadaye familia yote ilihama na kwenda kuishi kwa majirani ambapo wakiwa huko, mawe yaliendelea kurushwa ndipo mama mkwe akaondolewa na kupelekwa Dar es Salaam.

Anasema Machi 27 katika nyumba ya jirani ambayo mumewe alikuwa amepewa hifadhi iliungua moto.

Tukio hilo lilisababisha familia hiyo kukataliwa na wanakijiji na ndugu wa mama huyo kutotaka kuwaona watoto wake kwa kuhofia mauzauza kuwafuata.

“Tangu moto kuteketeza nyumba ya jirani ambako mume wangu alikuwa akiishi, aliondoka na kukimbilia kusikojulikana hadi leo hajaonekana.”

Elizabeth, mtoto wa mama huyo anasema tangu ilipoungua nyumba walipokuwa wamepewa hifadhi na baba yake, amekimbilia kwa bibi yake mzaa mama ambako ndiko anakoishi akiwa na mzazi wake.

Hata hivyo, anasema licha ya kukaribishwa katika makazi hayo baadhi ya ndugu wanahofia uwepo wake wakihofia kuandamwa na mauzauza hayo.

Kwa mujibu wa Elizabeth, ameshindwa kwenda shule na sasa yupo nyumbani na hata shuleni hofu dhidi ya matukio yanayomwandama ipo miongoni mwa wanafunzi na hata walimu wake.

Juhudi za kumpata Justine, hazikufanikiwa ambapo mkewe, Digna alisema tangu tukio la Machi 27 hajulikani alipo.



Chanzo: mwananchi.co.tz