Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yaiangukia Serikali kifo cha Mtanzania Zambia

Mtanzania Mwakyoma.jpeg Familia yaiangukia Serikali kifo cha Mtanzania Zambia

Sat, 16 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbeya. Siku moja baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii picha za mfanyabishara wa Zambia, ambaye ni raia wa Tanzania, Daudi Mwakyoma (40) akiteketea kwa moto, familia yake imeibuka na kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati ili mwili wake urejee nchini kwa maziko.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana Ijumaa, Septemba 15, 2023; Amin Mwakyoka, ambaye ni baba mzazi wa marehemu, amesema kama familia imesikitishwa na tukio hilo la kinyama kwa mtoto wake huku akieleza kuwepo kwa kizuizi kwa mwili kuruhusiwa kuja nchini.

“Mwanangu Daudi tangu akiwa hapa Mbeya, alikuwa akijihusisha na biashara ya viatu na alikuwa akisafirisha katika nchi mbalimbali na sasa alikuwa nchini Zambia tumeshangazwa kusikia ameuwawa kwa kuchomwa moto,” amesema.

Mwakyoma amesema wanaiomba Serikali ya awamu ya sita kuingilia kati kwa kuagiza ubalozi wa Zambia nchini, kusaidia ili mwili huo uweze kuruhusiwa kurejea nchini kwa ajili ya maziko iwe hata kama ni majivu au mifupa.

Kuhusu maisha yake

Amesema kuwa marehemu alikuwa msaada mkubwa kwenye familia yake na kwamba kifo chake kimeacha pengo kubwa na ambalo kimsingi halitafutika.

“Kuanza kwake biashara alianzia hapa Mbeya miaka iliyopita na alifundishwa na kaka yake ambaye kwa sasa ni marehemu, kwa kweli tumeumizwa sana na taarifa za kifo chake,” amesema.

Kwa upande wa Anania Mwakyoma, ambaye ni kaka wa marehemu, amesema kuwa tangu wamepata taarifa za kifo cha ndugu yao, hakuna kiongozi yeyote aliyeweza kutoa ufafanuzi juu ya hatua za kuchukuliwa ili kurejesha nchini mabaki ya mwili huo.

“Tunasikitishwa sana na ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwetu kwani, tumefuatilia bila mafanikio yoyote na hapa tulipo hatuelewi hatma ya mwili huo ni lini utaruhusiwa kuwasili nchini kwa maziko,” amesema.

Aidha amesema kuwa pia kuna uvumi juu ya kifo cha ndugu yao kuhusishwa na masuala fulani (ambayo hakuweka wazi) na kwamba huo ni wivu wa kibiashara tu.

“Ndugu yetu hayo mambo yanayozushwa juu ya kifo chake sio sahihi bali ni wivu wa kibiashara tu! Naomba Serikali ya Tanzania kuingilia kati tupewe mwili wa ndugu yetu, iwe mifupa, yawe majivu cha msingi azikwe kwenye ardhi ya Tanzania,” amesema.

Mama wa marehemu ambaye alishindwa kujitambulisha majina yake, baada ya kugubikwa na majonzi, amesema ameumizwa sana na kifo cha mwanaye Daudi kwani alikuwa ni tegemeo kubwa kwake.

“Mwanangu alikuwa mfanyabishara nchini Zambia, alikuwa akiuza viatu, mweeh, nitaishije mimi naomba Rais Samia Suluhu Hassan, anisaidie nione mwili wa mwanangu,” amesema huku akibubujikwa na machozi.

Semeni Athumani, jirani wa marehemu amesema kitendo alichofanyiwa marehemu Daudi ni cha kinyama, na kwamba enzi za uhai wake alikuwa ni kijana anayejituma katika utafutaji na alikuwa akiishi vizuri na majirani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live