Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya waziri yadai kuporwa kiwanja

Shamba Poc Familia ya waziri yadai kuporwa kiwanja

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utata umegubika umiliki wa eneo la ekari saba lililopo katika Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, baada ya familia ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango katika Serikali ya awamu ya nne, Jeremiah Sumari kudai kuporwa ardhi hiyo na Azim Dewji.

Wakati familia ya Sumari ikieleza hivyo, Dewji amefafanua namna alivyolinunua eneo hilo lililopo katika Mtaa wa Amani Gomvu.

Akizungumza jana kuhusu mgogoro huo, Miriamu Sumari alisema akiwa msimamizi wa mirathi, anatambua eneo hilo ni sehemu ya yale anayoyasimamia baada ya mumewe kufariki.

“Eneo hili nalifahamu mume wangu alilinunua mwaka 1992 tukiwa wote, tumejenga nyumba ndogo anayoishi mlinzi na nyingine haijakamilika, lakini tumekuwa na utaratibu wa kuja kulitembelea mara kwa mara hata kabla mume wangu hajafariki,” alisema Miriamu.

Taarifa ya kuchukuliwa kwa eneo hilo, alisema aliipata Februari 23 mwaka huu, baada ya kupigiwa simu na jirani yake, Mohamed Bhallo kumuuliza iwapo yeye ndiye anayeweka uzio.

Kutokana na taarifa hiyo, Miriamu anasema alilazimika kwenda na kukuta vijana wakiendelea na ujenzi wa nguzo za uzio.

“Nilipowauliza walinijibu wameagizwa lakini hawakumtaja mhusika, nilipoangalia nyaraka za kibali cha ujenzi walizokuwa nazo nikagundua zimeandikwa Azim Dewji,” alisema.

Hata hivyo, anasema kukosekana kwa hati ya eneo hilo kunatokana na mgogoro wa sehemu ndogo aliyotakiwa amalizane na jirani yake ndipo apimiwe.

Juma Mussa ambaye ni mlinzi katika eneo hilo, alisema ameifanya kazi hiyo tangu mwaka 2017 alipoajiriwa na Miriamu na tangu kipindi hicho hakuwahi kumwona mwingine yeyote akidai anaimiliki ardhi hiyo.

“Changamoto iliyokuwepo hapa walikuwa wanakuja watu kuulizia kama eneo hili linauzwa, tuliweka vibao vya kuonyesha kuwa eneo hili haliuzwi, tunashangaa wamekuja hawa wanaanza kuweka uzio,” alisema Mussa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mchangani lilipo eneo hilo, Waziri Yassin alisema ni vigumu kwake kueleza uhalali wa eneo hilo kwa kuwa ni muda mrefu sasa hayupo kazini.

Lakini, alisema anakumbuka kuwa Miriamu aliwahi kumtambulisha kijana kwake, akimweleza kuwa ni mlinzi wake katika eneo hilo.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Dewji alisema amenunua eneo hilo kwa John Mrowa Daudi kwa kufuata taratibu zote za kisheria na iwapo kuna malalamiko utaratibu ufuatwe.

Wakati anataka kununua, alibainisha kuwa alianza kwa kuiandikia barua Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kujua uhalali wake na akaelezwa anaweza kuendelea na mipango yake.

“Baada ya kujiridhisha nilifuata taratibu za kununua kiwanja hiki kilichokuwa mali ya John Mrowa na kama yeye ni mmiliki kwa nini hadi leo hajapata hati,” alisema Dewji, ambaye ni mfanyabiashara maarufu nchini.

Hata hivyo, jitihada za kumpata Daudi, aliyemuuzia Dewji eneo hilo hazijafanikiwa, kwani maofisa wa ofisi ya Serikali za Mtaa hawamfahamu mtu huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live