Siku moja baada ya Jeshi la Magereza kufafanua kifo cha Sheikh Said Ulatule (80), aliyedaiwa kufia katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam, familia ya sheikh huyo imeendelea kuikomalia Serikali wakitaka haki itendeke.
Juzi katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Magereza Dar es Salaam, George Wambura ilieleza kuwa kifo cha Sheikh Said kilichotokea Machi 4, kilichangiwa na shinikizo la moyo uliokuwa ukimsumbua tangu mwaka 2017 alipoingia gerezani hapo na mara ya mwisho kuhudhuria kliniki kupata matibabu ilikuwa Desemba 3, 2022.
Hata hivyo, jana ndugu wa marehemu Sheikh Said aliyefahamika kwa jina la Ulatule Usowasimba kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema matarajio yao baada ya kifo cha ndugu yao viongozi wangelifuatilia suala hilo ambalo linagusa haki na misingi ya raia.
“Serikali yetu sikivu ihakikishe haki inatendeka, si sahihi kumchukua mtu katika familia akiwa na afya njema kisha kurejesha maiti,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Sheikh Said aliwekwa gerezani tangu mwaka 2016, bila kupewa haki ya kujitetea na kuishia kufia mikononi mwa dola.
Akielezea ilivyokuwa katika mazishi ya Sheikh Said yaliyofanyika Machi 6, 2023, Katibu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisema kifo cha Sheikh huyo kilitokea Machi 4 mwaka huu, wakati Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Maghimbi akiwa gerezani hapo kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu.