Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya sheikh anayedaiwa kutekwa Mwanza njiapanda

32307 Pic+familia Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Familia ya Sheikh Bashir Gora imesema imeathirika kwa mambo mengi katika kipindi hiki ambacho inakosa uwepo wake.

Sheikh Gora, ambaye ni mkuu wa Chuo cha Kiislamu Nyakato jijini hapa alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Desemba 6, baada ya kijana mmoja kwenda chuoni hapo kuulizia nafasi za kujiunga kwa ajili ya mdogo wake.

Akizungumza na Mwananchi jana, mke mdogo wa Sheikh Gora, Farida Rashid alisema kwa sasa wanapitia katika wakati mgumu.

“Kama ni kuathirika ni mambo mengi tumeathirika nayo kwa sababu hakuna msaada wowote tunaoupata, hatuna chakula inabidi mimi nitafute kazi ya kufanya na nilikuwa mama wa nyumbani,” alisema.

“Lakini pia tunapokosa mlezi wa familia tunapata wakati mgumu kwa sababu yeye ndiye kila kitu.”

Hata hivyo alisema, “Tunachoamini Mwenyezi Mungu alichopanga hakuna anayeweza kukipangua, kama alipanga atakamatwa na sisi tutateseka basi hizi ni sababu zake, kikubwa tunazidi kumuomba apatikane japo hatujajua lini.”

“Labda wanaweza kuona huruma jinsi familia inavyoathirika wakamrudisha.”

Naye mdogo wa Sheikh Gora, Khalili Gora alisema wana imani kubwa na vyombo vya dola kupatikana kwa ndugu yao. “Hatujakata tamaa, vyombo vyetu vya dola tunaamini vinafanya kazi yake kuhakikisha anapatikana,” alisema Khalili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema wanaendelea kumsaka sheikh huyo na wanaamini atapatikana.

Anavyodaiwa kutekwa

Kwa mujibu wa Sadick Mchola, katibu wa taasisi inayomiliki chuo hicho, shule ya awali, msingi na sekondari ya Nyakato Islamic, alisema kabla ya Sheikh Gora kuchukuliwa aliingia kijana ofisini chuoni hapo akidai anataka fomu ya kujiunga. Baada ya kuambiwa zitatolewa Januari aliondoka na kurudi mara kadhaa huku akitaka pia fomu kwa ajili ya sekondari.

Baada ya kupewa fomu hiyo alisindikizwa na Sheikh Gora wakielekea nyuma ya chuo ambako kulikuwa na gari.

Alisema walipofika, alishuka kijana mwingine wakambeba Gora kwa nguvu na kumuingiza kwenye gari kisha kuliondoa kwa kasi. Hata hivyo aina ya gari na namba zake havikufahamika.



Chanzo: mwananchi.co.tz