Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya sheikh aliyetekwa Mwanza kufanya dua maalumu

34299 Pic+familia Tanzania Web Photo

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Ikiwa leo inatimia siku ya 25 tangu Sheikh Bashir Gora atoweke katika mazingira ya kutatanisha jijini Mwanza, familia yake inajiandaa kufanya dua maalumu kumuombea.

Jana, familia hiyo ililieleza Mwananchi kuwa imepanga kufanya dua maalumu kumwomba Mwenyezi Mungu kiongozi huyo wa dini apatikane akiwa hai.

Sheikh huyo ambaye pia ni mkuu wa Chuo cha Kiislamu Nyakato jijini hapa, anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Desemba 6, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Sadik Mchola, katibu wa taasisi inayomiliki chuo hicho, shule ya awali, msingi na Sekondari ya Nyakato Islamic, utekaji huo uliratibiwa na mtu asiyejulikana aliyefika chuoni hapo akidai kutafuta nafasi ya kujiunga na chuo.

Mchola alisema baada ya mtu huyo kukabidhiwa fomu alitoka akiwa ameongozana na Sheikh Gora aliyekuwa akimsindikiza, lakini walipofika nje kiongozi huyo alikamatwa na kuingizwa ndani ya gari kwa nguvu na kutokomea kusikojulikana.

Msemaji wa familia ya kiongozi huyo wa dini, Khalili Gora, alisema dua hiyo itafanyika leo nyumbani kwake eneo la Nyamhongolo wilayani Ilemela.

“Familia bado tuna imani na vyombo vya dola kuwa vinamtafuta na vitampata ndugu yetu akiwa hai na salama, nasi tumeamua kumuombea dua kuongeza nguvu katika jitihada za kupatikana kwake,” alisema Khalili.

Mke mdogo wa Sheikh Gora, Farida Rashid alisema licha ya kupata wakati mgumu kutokana na tukio la kutekwa kwa kiongozi huyo wa familia, bado wanaamini yuko salama na atarejea na kuungana nao.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alisema wanaendelea na upelelezi na kuwaomba watu wenye taarifa zinazoweza kusaidia kupatikana kwake wajitokeze.

Tukio hilo linafanana na lile la mtoto Idrissa Ally (13), aliyetekwa kwa staili ya ‘kimafia’ Septemba 26 mwaka jana, saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti, Dar es Salaam na leo ikiwa ni siku 96 ,bado hajulikani aliko.

Baba wa mtoto huyo, Ally Idd aliliambia Mwananchi kuwa hatachoka kumtafuta mwanaye huyo hadi atakampopatikana.



Chanzo: mwananchi.co.tz