Utata umeibuka baada ya familia ya mtoto, Ngatipa Parmao(17) anayedaiwa kuuawa kwa risasi na askari wa wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tnapa) kudai kuna njama zimefanywa kuondoa risasi mwilini kwa mtoto huyo katika hospitali ya awali alikokimbizwa kwa matibabu.
Familia ya mtoto huyo inasema majibu ya uchunguzi wa kitabibu uliofanywa jana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) inaonyesha matobo mawili yanayodaiwa ni ya risasi tumboni na mkono wa kulia.
Mtoto huyo ambaye ni wa jamii ya kifugaji ya kimaasai na mkazi wa kijiji cha Pangaroo, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro alifariki dunia juzi baada ya kudaiwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori katika hifadhi ya Mkomazi Julai 6.
Juzi, Mkuu wa Wilaya hiyo, Abdalah Mwaipaya alikiri kutokea kwa kifo cha mtoto huyo katika hospitali KCMC alikokimbizwa kwa ajili ya matibabu ambapo mpaka sasa Jeshi la polisi linamshikilia askari mmoja kwa kuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo Kamanda wa polisi mkoani humo, Simon Maigwa alisema kiutaratibu uchunguzi utakapokamilika jalada la mashtaka litaandaliwa na kupelekwa kwa mwanasheria mkuu wa Serikali.
Kauli ya familia
Akizungumza na Mwananchi kwa niaba ya familia jana akiwa KCMC baada ya uchunguzi wa mwili wa Ngatipa, kaka wa arehemu Daniel Imani aliiomba serikali kuingilia kati sakata hilo ili haki ya mtoto wao ipatikane kutokana na mashaka waliyo nayo.
“Baada ya mdogo wangu kupigwa risasi na askari wanyamapori alikimbizwa hospitali ya wilaya ya Same kutokana na hali yake kuwa mbaya na alifanyiwa upasuaji, chakushangaza wanatuambia hakuna risasi iliyoonekana, hatuna imani na haya majibu,” alisema
“Na mpaka tulipompeleka hospitali ya KCMC na kufariki jana (juzi), mwili umefanyiwa postmoterm na tumboni pamoja na mkono wake wa kulia kuna mashimo ya risasi na hakuna risasi iliyoonekana ila sisi tuna wasiwasi na hospitali ya Same ambapo ndio waliompokea mara ya kwanza,” alisema
Kaka huyo wa marehemu alisema,”sisi tunachoiomba serikali kwasababu mtoto wetu inajulikana amekufa, tunaomba iingilie kati ili wale wote waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria ili hali ya ndugu yetu ipatikane.”
Awali kaka wa marehemu alidai siku ya tukio wakati ndugu yao akiswaga ng’ombe karibu na eneo la mpakani alikutana na askari hao ambao walilazimisha kuingiza ng’ombe hifadhini na alipojaribu kuzuia alipigwa risasi ya tumbo.
Hata hivyo, Kamishna msaidizi wa uhifadhi Mkomazi, Emanuel Moirana alisema baada ya askari hao kukamata mifugo iliyokuwa ikiswagwa ndani ya hifadhi hiyo wananchi waliwavamia askari hao ambao walikuwa ni watano na kwamba wakati wakijihami walirusha risasi angani kwa kuwa wananchi hao walikuwa wamebeba masime.
“Taarifa nilizo nazo ni kwamba askari walikamata mifugo ndani ya hifadhi ndipo wananchi walipovamia na askari wakafyatua risasi ndipo ilipompata huyu mtoto kwa bahati mbaya kwenye zile purukushani,”alisema Moirana
“Kiutaratibu huwa mtu haruhusiwi kuingiza mifugo ndani ya hifadhi hivyo mifugo ikikamatwa huwa kuna taratibu zinafanywa lakini hawa wananchi wakawa wamewavamia askari,” alisema Moirana.