Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya anayedaiwa kuuawa na mumewe yafanya ibada kumshukuru Mungu

69796 Naomi+pic

Mon, 5 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika ibada ya shukrani iliyoandaliwa na familia ya Naomi Marijani anayedaiwa kuuawa na mumewe na mwili wake kuteketezwa kwa moto.

Inadaiwa kuwa mume huyo, Khamisi Luwongo ambaye tayari amefikishwa mahakamani  alimuua mkewe na baadaye kutumia magunia mawili ya mkaa kuchoma maiti yake na kisha kufukia majivu yake katika shamba lake lililoko Kijiji cha Marogoro kilichopo wilayani Mkuranga.

Kwa mujibu wa polisi, baadaye mume huyo alienda kituo cha polisi kutangaza kuwa mkewe, ambaye ni mama wa mtoto mmoja, ametoweka nyumbani kwake Gezaulole-Kigamboni tangu Mei 15, 2019.

Sampuli ya mabaki yanayodaiwa kuwa ya Naomi yanachunguzwa na Ofisi ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Ibada hiyo imefanyika leo Jumapili Agosti 4, 2019 nyumbani kwa kaka yake Naomi, Mbweni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumshukuru Mungu.

Waombolezaji wengi wameoneka wakiwa wamevalia mavazi meupe huku nyuso zao zikiwa na huzuni.

Habari zinazohusiana na hii

Wiseman Marijani, kaka yake Naomi amesema mbali na kumshukuru Mungu, pia wanamkabidhi suala hilo ili haki itendeke.

“Kwa hatua tulizopitia na jambo lenyewe lilivyo bila uwezo wa Mungu tusingeweza. Tumepanga tukutane kama familia na wote walioguswa tumshukuru Mungu ametutendea makuu.”

“Kupata ukweli wa kilichomtokea ndugu yetu na hata vyombo vya sheria kuingilia kati ni neema kubwa na ndiyo maana tunamshukuru huku tukimkabidhi hilo shauri akaendelee kuonyesha ukuu wake,” amesema

Wiseman ameeleza kuwa familia inaendelea kusubiri uamuzi wa mahakama kuhusu mabaki ya ndugu yake hadi pale itakapotoa ridhaa ya kisheria ya kuzika.

“Leo tumekutana ila mahakama itakapomaliza taratibu zake na kutukabidhi masalia tutaitana tena kama hivi ili tuweze kumzika ndugu yetu kwa heshima zote,” amesema Marijani.

Chanzo: mwananchi.co.tz