Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya Mkwawa yatoa tamko zito

85102 Pic+mkwawa Familia ya Mkwawa yatoa tamko zito

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa. Familia ya Chifu Mkwawa na mwenyekiti mila na desturi za Wahehe, Augustino Mkini wamepiga marufuku mtu yeyote kumwakilisha Chifu Adam Mkwawa II katika shughuli yoyote bila kamati ya wazee wa kimila kumteua.

Mzee Mkina alitoa agizo hilo jana akizungumza na wanahabari kutokana na mmoja wa wazee hao, Gerlad Malangalila kudaiwa kuwa na mazoea ya kujitambulisha kama ndiye chifu wa Wahehe na kushiriki shughuli za kichifu bila kumshirikisha Chifu Adam II.

Mkina alisema sintofahamu hiyo imekuja baada ya kituo kimoja cha televisheni kumwandika mzee Malangalila kama chifu wa Wahehe na kukitaka kukanusha taarifa na kuwaomba radhi kabila hilo.

“Kwenda katika shughuli za kichifu bila kumshirikisha chifu na kujitambulisha ndiye chifu ni kutaka kupindua au kusaliti uamuzi wa familia na kamati ya wazee wa kimila, hivyo kamati na familia ya chifu tunapiga marufuku mtu yeyote kumwakilisha chifu bila ruhusa ya Chifu Adam II au kamati ya wazee,” alisema Mkina.

Alisema tayari Chifu Adam II amefikisha umri wa kutambua mema na mabaya, hivyo kila itakapotafanyika shughuli ya Kihehe ya kimila mwenyewe atatakiwa kwenda asipoenda atamchagua mtu wa kumwakilisha. “Tumeona malangalila anahudhuria shughuli nyingi za Serikali jambo ambalo hatuna taarifa nalo, hivyo kutokumshirikisha Chifu Adam II ni kutangaza ufalme wake,” alisema Mkini.

Dada yake Chifu Adam II, Fatma Mkwawa alisema familia na wazee wa kimila imepokea malalamiko mengi ya wananchi, hivyo wameona si jambo zuri kukaa kimya.

Naye ofisa utamaduni manispaa ya Iringa, Merisina Ngowi alisema Serikali ipewe taarifa kuwa Chifu Adam II tayari amefikisha umri wa kujishughulisha na cheo hicho.

Chanzo: mwananchi.co.tz