Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya Membe yampa siku 7 daktari “Atueleze chanzo cha kifo cha ndugu yetu”

Membe Daktari Familia ya Membe yampa siku 7 daktari

Fri, 26 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Familia ya ya aliyewahi kuwa Waziri wa mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Kamilius Membe imemkana daktari aliyejitokeza siku ya msiba na kusema kuwa ni daktari wa familia na daktari binafsi wa Membe huku ikidai kuwa alichokizungumza kuhusu chanzo cha kifo cha ndugu yao hawakubaliani nacho.

Akizungumzia hilo mdogo wa marehemu aitwaye Steven Kamilius Membe ametoa siku saba kwa daktari huyo aliyejitambulisha kwa jina la Profesa haruni Nyagoli kujitokeza hadharani na kuwaeleza Watanzania maswali kadhaa ambayo ameyaainisha huku akidai pia kuwa wanayo mashaka kwa nini daktari huyo aliwahi kutoa taarifa ya msiba pasi na kuwashirikisha ndugu wa marehemu.

“Kaka yetu Membe alikuwa India ambapo alikwenda kutibiwa jicho lake la kulia, lilikuwa lina uwezo wa “kuona kwa asilimia 30 tu na la kushoto asilimia 75, hivyo alilazimika kufanyiwa upasuaji na kulitibu kisha akaambiwa arudi kule baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na lile jicho la pili.

“Akiwa India alifanya vipimo vingine vya mwili wake na kubainika kuwa alikuwa na stone kidney ambao ni ugongwa wa kawaida (kijiwe kwenye figo), hakuhitaji upasuaji, alipewa dawa akanmeza na akawa vizuri akarejea nyumbani Tanzania mpaka hapa kijijini Rondo akiwa mzima wa afya, baadaye akaenda Dar.

“Mambo mengi yamesemwa sana juu ya chanzo cha kifo hiki, tumeona mtu akijiita daktarti wa familia akielezea ghafla kilichosababisha kifo cha kaka yetu, tunashangaa sana.

“Hakukuwa na ugonjwa wowote sugu wa Membe unaofahamika kwangu ama kwa familia. Wakati tunajiandaa kuhoji nini kimetokea, kabla sijaondoka hata hapa kijini kwenda Dar msibani, dakatri ambaye hata jina lake simjui, hata akija mbele ya macho yangu siwezi kumjua, akataja chanzo cha kifo cha kaka yetu.

“Nilikuwa na maswali mengi sana, kwa nini haraka ya kutangaza kifo chake, huyu daktari nisiyemfahamu kwa sura ama kwa jina alipata wapi idhini ya kutangaza nini kilichotokea, sio daktari wa familia na familia haimjui, sio hapa Rondo ama kule Dar alikokuwa akiishi Membe.

“Maelezo niliyopata ni kwamba kaka yangu siku ya Alhamisi, alijipeleka mwenyewe akiwa anatembea, akasema ikifika saa 10 alfajiri anakuwa akijisikia kukohoa na kubana pumzi, Hospitali ya Kairuki wakamfanyia vipimo na kumpa dawa, wakajiridhisha kuwa hakuwa kwenye hali yoyote ya hatari na kwamba hakukuwa na uhmihimu wa kumlaza, hivyo akaruhusiwa kuondoka.

“Alielekezwa arudi siku ya pili yake kwa ajili ya kupeleka sampuli ya mkojo ili kufanya uchunguzi kuhusu tatizo la kidney stone. Aliporudi nyumbani, ilipofika saa 10 alfajiri akapata hali ile ile, akapelekwa hospitali akiwa hajitambui, na baada ya hapo ilipofika saa 2 asubuhi alifikwa na umauti.

“Cha ajabu, saa 4 asubuhi, huyo mtu anayejiita daktari akatangaza kilichomuua, mimi na familia tuna maswali mengi sana kuhusu kifo hiki, mpaka sasa hatujui nini chanzo cha kifo cha mpendwa wetu. Nikiwa msibani pale dar nilimtafuta lakini sikumpata labda kwa vile simjui nay eye hanijui, nilijikita na shughuli za kumpumzisha kaka yangu kwenye nyumba yake ya milele.

“Sasa ninampa siku saba daktari huyu ajitokeze kujibu maswali haya, alipata wapi idhini ya kuziongelea habari za matibabu za mgonjwa, kwa sababu sheria hazimruhusu kufanya hivyo labda amepewa kibali cha familia au ameitwa mahakamani.

“Kingine atuambie, ni dokta wa familia ipi, kule alikozaliwa Membe au familia ya Membe kwa maana ya mkewe na watoto. Hata hayo aliyosema kwamba yalisababisha kifo cha Membe si ya kweli, ameidanganya taaluma.

“Je, alitumia utafiti gani kusema hayo, alifanya postmortem baada ya kifo, alipata kibali cha nani? Lazima aje na vigezo. Huyu daktari ana funguo ya baadhi ya maswali, atatueleza nini kilitokea. Daktari wa familia tunayemjua sisi ni Dokta Onesmo Kaganda ambaye ni Mganga Mkuu wa Kairuki Hospital na ndiye slipokea pale hositali, sasa huyu alitokea wapi?

“Sisi kama familia tunasema chanzo cha kifo cha kaka yetu hakijulikani, tunashangaa anasema kifo chake kilisababishwa na virusi mgando wanapelekea tatizo la pulmonary embolism. Hili ni tatizo ambalo ni mzuio tu wa damu kwenda kwenye mapafu kubadilishana oksjen na carbon monoxide tu, na damu hiyo inakuwa inatokea miguuni kupitia mishipa inaitwa deep vein thrombosis.

“Lakini anashindwa kutuambia kuwa tatizo hili linaweza pia kusababishwa na sumu inayoitwa acute pulmonary poisoning (sumu kwenye mapafu), kwa nini anatuzuia kufikiria hilo. Sayansi haiondoi mnonong’ono kwa kutumia mnong’ono na sio badala yake inajibiwa kwa sayansi. Sasa tunamtaka ajitokeze ndani ya siku saba aeleze,” amesema Steven Membe.

Awali siku msiba, Profesa Haruni Egoli, ambaye alisema mbele ya wanahabari kuwa ni Daktari mwandamizi na msahuri wa maradhi ya ndani na maradhi ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili, na daktari wa familia na daktari binafsi wa Membe alisema.

"Kwa kifupi niseme, Mh. Membe amekuwa mzima kwa miaka mingi, hajawahi kuwa na tatizo lolote la magonjwa sugu kama ya Sukari, Presha, Magonjwa ya moyo hajawahi kuwa nayo.

"Kilichotokea ni kwamba amepata maambukizi ya ghafla ya mfumo wa mapafu hewa, ambayo imepelekea akapata mgando wa damu kuwa nzito na kusababisha mapafu kushindwa kupeleka oxygen (kitaalam inaitwa pulmonary embolism)".

"Hii inatokea mara kwa mara sana kwa mtu anayepata maradhi ya pneumonia ambayo husababisha damu kuganda.

"Kwa hiyo niondoe tafrani na mkanganyiko unaendelea huko mtaani kwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba huenda Membe ameuawa au amenyweshwa sumu, au matatizo mengine hapana hiyo ni hali iliyopo, nalieleza Taifa, tatizo hili anaweza kupata mtu yeyote hata mimi".

"Membe amepumzika yuko katika mazingira hayo, hakuna kingine cha kusema nje ya sababu ya hiyo ya kifo," amesema Daktari huyo.

Bernard Membe alifariki dunia Mei 12, 2023 majira ya saa 2 asubuhi wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla na alizikwa kijijini kwao Rondo, Mtama mkoani Lindi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live