Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia ya M-NEC wa CCM yamlilia Lukuvi

33129 BIBI+YAKE+PIC Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Familia ya mjumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, marehemu Asha Kabelele maarufu Mama Chiliko imemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati mgogoro wa ardhi kati yao na uongozi wa Halmashauri ya Ilemela.

Mmoja kati ya wanafamilia ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake amelalamikia uongozi wa halmashauri hiyo kumega viwanja viwili vya familia hiyo eneo la mtaa wa Ghana Kota jijini Mwanza.

Mama Chiliko ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) alifariki dunia mwaka 2011 na ameacha familia inayoendelea kuishi katika nyumba aliyomiliki mtaa huo.

Akizungumza na Mwananchi jana, mwanafamilia huyo alisema halmashauri hiyo imechukua kipande kutoka ploti namba 492 na kipande kingine kutoka kiwanja cha nyumba wanayoishi ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na kujimilikisha hati kisheria ikiwa ni kinyume cha maagizo ya Serikali.

Hivi karibuni, Lukuvi aliagiza wakazi wanaoishi katika nyumba za kota kwenye mikoa 20 kutoondolewa hadi utaratibu wa kupanga na kumilikisha utakapopangwa kwa mara nyingine na Serikali.

Waziri Lukuvi jana aliitaka familia hiyo kuwasilisha malalamiko yake katika ofisi za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), akisema ardhi na nyumba zote za kota nchini ziko chini ya umiliki wa wakala huo.

“Kama ni zile kota za Serikali ardhi na majumba tumeimilikisha TBA, wapangaji waliokuwapo wanabakia walewale lakini watakuwa tenant (wapangaji) wa TBA siyo halmashauri tena,” alisema Lukuvi.

Hata hivyo, mwanafamilia huyo alidai kufika ofisi za TBA ambako alielezwa mipaka ya wakala huo iko katika upande wa kiwanja kilichomegwa kutoka NHC pekee.

“Tumeenda TBA wakasema wao wanahusika na kipande cha NHC, wakasema tuangalie endapo ujenzi wao utaingilia eneo la NHC ndiyo watahusika, lakini tunashangaa wameshaingia eneo la NHC ushahidi tunao wa picha, tunaomba Serikali iingilie kati,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliagiza wakazi hao kufika ofisini kwake wakiwa na ushahidi wa nyaraka zinazothibitisha kumiliki maeneo hayo kisheria, lakini kama ni wapangaji wa TBA anatakiwa TBA mwenye mali ndiyo alalamike.



Chanzo: mwananchi.co.tz