Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia kijana aliyezikwa porini yataka uchunguzi

Fidia Kuzikwa Porini.png Familia kijana aliyezikwa porini yataka uchunguzi

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakati Serikali imeunda kamati ya watu saba kuchunguza kifo chenye utata cha kijana Enos Elias (20), familia ya kijana huyo imeomba Serikali kuweka wazi sababu za kifo hicho, wahusika na hatua za kisheria zilizochukuliwa.

Familia imetoa kilio hicho jana kupitia kwa mama mzazi wa kijana huyo, Juliet Joseph alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake katika Kijiji cha Ilabilo, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, akisisitiza kuwa yeye na familia nzima wanaamini Enos alifikwa na mauti akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa vyombo na taasisi za Serikali.

Kutokana na utata uliogubika kifo cha Enos, ambaye mwili wake ulikutwa umezikwa katika pori la Kichacha eneo la Kijiji cha Chilambo Wilaya ya Kakonko, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mwanamvua Mrindoko ameunda kamati ya watu saba kuchunguza sababu, mazingira na wahusika wa kifo hicho.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Ofisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Andrew Mrama alisema kamati hiyo ambayo kiongozi wake na wajumbe hawakutajwa, iliundwa Novemba 15 na tayari imeanza kazi.

Sambamba na hatua hizo, Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, David Misime limetangaza kuanzisha uchunguzi kubaini sababu, mazingira na wahusika wa kifo cha Enos na limewaomba wananchi wenye taarifa kujitokeza kusaidia uchunguzi huo.

Hatua ya mwisho

Mama huyo wa marehemu, aliwaeleza waandishi wa habari nyumbani kwake jana kuwa anaamini mtoto wake amefariki akiwa mikononi mwa maofisa wa vyombo na taasisi za Serikali kwa sababu mara ya mwisho alipowasiliana naye aliwajulisha kuwa ameshikiliwa na askari wa Uhamiaji.

“Hadi sasa najiuliza mtoto wangu aliwakosea nini hadi wakaamua kumuua na kwenda kumzika kimya kimya porini? Naiomba Serikali inisaidie kujua chanzo na sababu za kifo cha mtoto wangu na wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Juliet.

Angle Elias, dada wa marehemu aliyezungumza na Enos mara ya mwisho Ijumaa ya Oktoba 28, mwaka huu alisema: “Nilikuwa shambani mimi na mama; kaka akanipigia simu akiniomba nimtumie namba ya NIDA (kitambulisho cha Taifa) ya mama ili awathibitishie maofisa Uhamiaji kwamba yeye ni Mtanzania na si Mrundi,” alisema.

Alisema kwa sababu namba hiyo ilikuwa imeandikwa kwenye karatasi ambayo ilikuwa nyumbani wakati huo, mama yao alilazimika kwenda kuchukua karatasi hiyo ili wamtumie Enos; lengo ambalo halikufanikiwa baada ya simu yake kutopatikana hewani.

“Wakati anazungumza nami kwa simu, kaka alinisisitizia nimtumie namba ya Nida ya mama ili aondokane na mateso baada ya kukamatwa Ijumaa (Oktoba 27, 2023) na kulala mahabusu ya Polisi mjini Kakonko akidaiwa kuwa si raia,” alisema Angel.

Baada ya simu ya Enos kutopatikana hewani, Angel aliwasiliana na kaka yao mwingine aliyemtaja kwa jina la Leopold Kisondoka, aliyeenda hadi Kituo cha Polisi Kakonko kumtafuta Enos hadi bila mafanikio.

“Kutokana na maelezo ya kaka kwamba alikuwa anashikiliwa na maofisa Uhamiaji na alilala kituo cha polisi, mimi na ndugu wengine tulienda ofisi za Uhamiaji na Kituo cha Polisi Kakonko ambako kote wahusika walikana kumshikilia wala kuwa na taarifa zake,” alisema Angel Licha ya ndugu kuendelea kufuatilia mfululizo kuanzia Jumapili ya Oktoba 29, 2023 hadi Jumanne Oktoba 30, 2023, alisema maofisa wa taasisi hizo walishikilia msimamo wa kutomshikilia wala kuwa taarifa za Enos.

Kwa mujibu wa Angel, familia iliendelea kufuatilia suala hilo kituo cha polisi na Jumatano Oktoba 31, 2023 ilipata taarifa kutoka kwa mmoja wa maofisa kuwa ni kweli Enos alikamatwa na maofisa Uhamiaji ambao walienda kumhifadhi kwenye mahabusu kituoni hapo usiku wa Ijumaa Oktoba 27, mwaka huu.

“Yule askari alitujulisha kuwa ndugu yetu alikabidhiwa kwa maofisa Uhamiaji asubuhi ya Jumamosi tarehe 28, 2023. Baada ya taarifa zile tulienda ofisi ya OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) ya Kakonko ambaye aliongozana nasi hadi ofisa za Uhamiaji kufuatilia suala hilo,” alisema.

“Maofisa wa Uhamiaji tuliowakuta walikiri mbele ya OCD kuwa ni kweli walimshikilia Enos lakini walishamwachia na hawajui alipoenda. Tulishangazwa na taarifa hizo kwa sababu ni karibia wiki nzima walikuwa wanakana kumshikilia wala kuwa na taarifa zake.”

Alisema ilipofika Ijumaa ya Novemba 3, 2023, walipigiwa simu wakitakiwa kufika Kituo cha Polisi Kakonko ambako walielezwa kuwa kuna kaburi jipya limebainika katika pori la Kichacha, umbali wa zaidi ya kilomita 25 kutoka Kakonko mjini.

“Tuliongozana na askari hadi porini na baada ya kaburi kufukuliwa na mwili kutolewa, mama aliutambua kuwa ni wa marehemu Enos, kutokana na alama iliyokuwa nayo kwenye meno,’’ alisema.

Wagomea mwili

William Sabakwisi, baba mdogo wa marehemu Enos alisema kutokana na utata wa kifo hicho na kitendo cha Jeshi la Polisi kumshikilia mmoja wa ndugu aliyemtaja kwa jina la Leopold Kisondoka kwa mahojiano baada ya kubainika kuwasiliana mara kadhaa na Enos kabla ya kifo chake, familia iligoma kuchukua mwili huo kushinikiza uchunguzi.

“Kwanza, familia ilichukizwa jinsi Polisi na Uhamiaji walivyowazungusha kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Enos; pili, familia ilihisi kitendo cha kumshikilia Leopold ambaye ndiye alikuwa kinara wa kumtafuta Enos, zilikuwa njama ya kumbambikia kesi ili kuwalinda wahusika,” alisema Sabakwisi.

Alisema baada ya majadiliano, polisi walimwachia Leopold na familia ikakubali kuchukua mwili kwa masharti kuwa mazishi hayatafanyika hadi Serikali itoe taarifa za sababu, mazingira na wahusika wa kifo hicho. Licha ya familia ikiungwa mkono na wanakijiji wa Ilabilo kutangaza kugoma kuzika, ndugu wachache pamoja na maofisa wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali walishiriki mazishi ya Enos yaliyofanyika kwenye makaburi ya umma kijijini hapo Novemba 14, 2023.

Zitto ahani msiba

Akizungumza na familia ya marehemu Enos alipofika kuhani msiba huo jana, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama hicho kitashirikiana bega kwa bega na familia kufuatilia hadi sababu, mazingira na wahusika wa kifo cha kijana huyo.

“Katika hili sisi ACT-Wazalendo kama taasisi, tunalitaka Jeshi la Polisi litimize wajibu kwa kuchunguza kwa kina kifo hiki na wahusika wote wafikishwe mahakamani kwa sababu hakuna sababu iwayo yote inayohalalisha kilichotokea,” alisema Zitto.

Kiongozi huyo aliye kwenye ziara ya kichama katika majimbo ya Mkoa wa Kigoma alilitaka Jeshi la Polisi kuanza uchunguzi kwa kufuatilia mawasiliano ya simu ya marehemu na maelezo ya ndugu aliowasiliana nao akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa Serikali kabla ya kutoweka na mwili wake kukutwa umezikwa porini.

Chanzo: mwanachidigital