Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia Dar yasusa maiti ya ndugu Muhimbili, yalia na Jeshi la Polisi

12542 Familia+pic TanzaniaWeb

Sat, 18 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Familia ya Kindamba ya jijini hapa, imegoma kuuchukua mwili wa ndugu yao, Salum Kindamba aliyefariki dunia wiki iliyopita kutokana na utata wa ripoti iliyotolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kuhusu chanzo cha kifo chake wanachokihusisha na kupigwa risasi na polisi.

Juhudi za kuwapata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa hazikuzaa matunda jana.

Mwananchi lilipowakosa lilimtafuta msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa aliyeelekeza watafutwe makamanda hao.

“Kuhusu suala hilo mtafute kamanda wa Kanda Maalumu atalishughulikia,” alisema Mwakalukwa baada ya kuelezwa kuwa juhudi za kumpata Kamanda Lukula zimegonga mwamba mara kadhaa.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Omary Kindamba alisema Salum alifariki dunia Agosti 9, akiwa katika baa iliyopo eneo la Jet Rumo na rafiki zake. “Mashuhuda wa tukio hilo wameona na kutusimulia kila kitu,” alisema Omary.

“Unajua ilikuwa hivi, hawa jamaa (polisi) walikwenda kwenye baa hiyo na siku hiyo huyu ndugu yetu alikuwa amebeba begi ambalo ndani yake kulikuwa na Sh9 milioni.

“Sasa siku za nyuma ilisemekana kuwa watu walikuwa wakipendelea kwenda kwenye eneo hilo kwa ajili ya kugawana fedha na polisi walikuwa wamearifiwa juu ya mwenendo huo na mara kwa mara walikuwa wakifika kupiga doria.”

Alidai wakati Salum na rafiki zake watatu wakiwa kwenye baa hiyo ghafla walizingirwa na polisi ambao waliwaamuru kuwa chini ya ulinzi.

Alisema ndugu yao hakutii amri hiyo na kuanza kukimbia, ndipo alipomiminiwa risasi zinazodaiwa kusababisha kifo chake.

“Sasa baada ya tukio hilo ndipo tulipofuatilia katika Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako baadaye tulifahamishwa kweli ndugu yetu alikuwa amefariki dunia na mwili wake ulihifadhiwa Hospitali ya Temeke,” alisema Omary.

Alisema taarifa walizopewa kituoni hapo zilieleza kuwa alikuwa amepigwa na kitu chenye ncha kali na baada ya mabishano na polisi wakakubaliana kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu. “Siku ya pili tulivyokwenda tukaambiwa amefariki (dunia) kutokana na mshtuko uliosababishwa na kitu cha ncha kali.”

Alidai familia haikukubaliana na maelezo yaliyotolewa na madaktari wa Hospitali ya Muhimbili na wamesusa kuchukua mwili wa marehemu hadi pale watakapopewa taarifa ‘halisi ya kilichosababisha kifo chake’.

“Wanasema ripoti imepelekwa polisi Chang’ombe na kule hawataki kutupatia na sisi tumeamua hatuchukui mwili wa marehemu hata zikipita siku 40.”

Muhimbili wazungumza

Akizungumzia sakata hilo, Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa wa MNH, Dk Praxeda Ogweyo alisema kwa kawaida hospitali huandika ripoti kamili ya kifo (postmortem), lakini ndugu hupewa kibali cha kuzika ambacho kinakuwa na taarifa kwa ufupi.

“Sisi tulitoa kile kibali chenye taarifa fupi, lakini ripoti kamili tunaipeleka polisi ili mtu ajue sababu ya kifo tuliyoiandika ni lazima apate ripoti kamili,” alisema Ogweyo ambaye kitengo chake pia huhusika na uchunguzi wa sababu za vifo.

Alisema kwa kawaida kibali huandikwa sababu ya awali ya kifo na kibali cha mazishi walichopewa ndugu wa Salum kinaeleza kuwa alifariki kwa mshtuko.

Hata hivyo, alisema ripoti kamili inafafanua kwa kina zaidi juu ya kifo. Dk Ogweyo alisema walichosema polisi kulingana na ripoti yao ndicho wao (MNH) walichokiandika.

Ndugu msibani

Mwananachi jana lilifika nyumbani kwa kaka wa marehemu eneo la Kipawa na kuwakuta ndugu wakiwa wamekusanyika huku wakiendelea kuomboleza. Ndugu hao waliendelea kusisitiza kuwa hawapo tayari kuchukua mwili wa marehemu hadi watakapojiridhisha juu ya mazingira ya kifo chake.

“Mwili hatuuchukui mpaka tujue sababu halisi,” alisema mmoja wa ndugu ambaye hakutaka kutajwa jina lake. Salum ameacha mke na watoto wanne wakiwamo mapacha wenye umri wa miaka minne.

Chanzo: mwananchi.co.tz